SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 24 Mei 2016

T media news

WACHEZAJI WA BONGO MMEJIFUNZA NINI KUTOKANA NA MAFANIKIO YA MA-PRO WA VPL?

Baada ya msimu wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara kumalizika, tunapata fursa ya kufanya tathmini ya mambo mbalimbali yaliyojiri ndano ya msimu mzima.

 leo tutaangalia mafanikio waliyopata wachezaji wa kigeni ukilinganisha na wale wazalendo.

Kumekuwa na ongezeko la wachezaji wawili walioruhusiwa kwa mujibu wa kanuni za msimu huu. Awali timu ziliruhusiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni lakini sasa wameongezwa hadi saba na hii ilikuwa ni ombi maalum kulingana na madai ya vilabu vinavyoshiriki michuano ya kimataifa.

Lakini bado ni vilabu vichache vyenye uwezo wa kuwalipa nyota hao. Simba, Yanga na Azam ndiyo vilabu pekee vilivyoweza kusajili idadi ya wachezaji saba wa kigeni.

Tuachane na hayo na turejee kwenye hoja ya msingi ya mafanikio wanayopata wachezaji wa kigeni ukilinganisha na wazalendo. Je wachezaji wetu wa nyumbani kuna kitu wanajifunza?

Magolikipa

Vicent Agban golikipa wa Simba SC unaweza ukasema amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani amecheza mechi nyingi kuliko mpinzani wake Manyika Jr.

Awali Manyika Jr alianza kuaminiwa na klabu yake na kufanikiwa kucheza mechi kubwa ya watani wa jadi Simba vs Yanga huku Ivo Mapunda akiwa benchi wakati huo Ivo akiwa Simba.

Lakini ujio wa golikipa raia wa Ivory Coast ndani ya Simba umempoteza Manyika kabisa katika nafasi yake.

Walinzi: Wawa, Bosou, Juuko

Walinzi hawa wamekuwa tegemeo kwenye vikosi vyao kutokana na mchango wanaoutoa wakiwa uwanjani.

Wawa amekuwa muhimili mkubwa kwenye safu ya ulinzi ya Azam. Mfumo wa 3-5-3 uliokuwa ukitumiwa na mkufunzi Stewart Hall, Wawa alikuwa nguzo muhimu kabla ya kupata majeraha.

Agrey Morris, Said Mourad na David Mwantika walikuwa wakibadilishana nafasi lakini Wawa aliendelea kuwa kiongozi wao.

Juuko Murshid wa Simba SC pia amekuwa muhimili kwenye klabu yake licha ya kiwango chake kushuka siku za hivi karibuni.

Amecheza mechi nyingi za VPL huku akibadilishiwa partners, Hassan Isihaka, Abdi Banda, Novatus Rufunga na mara kadhaa alicheza na Justice Majabvi. Beki huyu mganda aliaminiwa na walimu wote waliopita Simba.

Vicent Bosou ni kisiki kingi cha Yanga ambacho kimewaziba midomo wengi waliokuwa wakipiga kelele siku za awali.

Uvumilivu wa Bosou na kujitambua kumethibitisha kwamba jamaa ni professional na anajua anafanya nini.

Alianzia benchi lakini bado aliamini ipo siku maisha yatabadilika. Kuumia kwa nahodha wa Nadir Haroub ilikua ni fursa ya yeye kufanya yake. Leo unapolitaja jina la Bosou kwenye kikosi cha Yanga unagusa mchezaji muhimu kwenye safu yao ya ulinzi kutokana na kudhihirisha ubora wake.

Viungo: Justice Majabvi, Kamusoko, Niyonzima, Mugiraneza

Hakuna asiyeijua shghuli ya kiungo mkabaji Justice Majabvi ambaye mara nyingi amekuwa kivuli lakini akifanya kazi kubwa ya kuilinda safu yake ya ulinzi.

Kamusoko ni kipenzi cha wanajangwani kwa sasa, analipa thamani yake uwanjani. Uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi, kukaba, kufunga na hata kuanzisha mashambulizi umeendelea kumpa nafasi kwenye kikosi cha Yanga.

Uwepo wake Yanga unazima nafasi za Telela pamoja na Said Makapu.

Haruna Niyonzima mchezesha timu hakuna mtanzania asiyejua uwezo wa mnyarwanda huyu.

Kuna wakati Yanga walimpiga chini lakini baadaye wakamrejesha tena na hakuna anayewalaumu kwa kumrejesha fundi huyu kutokana na uwezo wake wa kuamua timu icheze kwa mtindo gani.

Mugiraneza pia unaweza usione kazi yake pale Azam lakini Hall ndiye anajua umuhimu wa kiungo huyu wa zamani wa APR ya Rwanda.

Anaweza kukaba na ni mzuri kwa mipira ya juu, mara nyingi amekuwa akitumiwa kwenye kikosi cha kwanza kabla ya kupata majeraha ambayo yametoa mwanya mwingine kwa Mudathir Yahya kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.

Washambuliaji: Amis Tambwe, Hamisi Kiiza, Donald Kamusoko

Tambwe ndiyo amebeba kiatu cha ufungaji bora msimu huu akiwa na mabao 21baada ya mechi 30 kumalizika.

Ni mafanikio makubwa kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba baye huu ni msimu wake wa pili Yanga lakini ukiwa ni msimu wa tatu VPL.

Mpachika mabao mwingine wa kigeni ni Hamisi Kiiza kutoka klabu ya Simba na timu ya taifa ya Uganda.
Mabao yake 19 yanamfanya kumaliza nyuma ya Tambwe kwa magoli mawili. Kiiza alianza vizuri msimu na hadi kuongoza mbio hizo za kuwania ufungaji bora kabla ya mambo kubadilika kwenye klabu yake na kukosekana kwenye mechi za mwishoni mwa ligi.

Magoli 19 ni mafanikio kwa Kiiza kutokana na nafasi yake ukizingatia amechwa kwa magoli mawili tu na mfungaji bora wa msimu huu.

Donald Ngoma mwiba wa mabeki wengi kwenye ligi msimu huu. Akiwaamefanikiwa kufunga magoli 17 mabao mawili nyuma ya Kiiza na manne nyuma ya mfungaji bora Amis Tambwe, Ngoma amefanikiwa kwa kiasi kikubwa ndani ya msimu wake wa kwanza VPL.

Paul Nonga, Matheo Anthony na Malimi Busungu ni washambulizi wazalendo kwenye kikosi cha Yanga, watatu hawa wamekuwa hawapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ubora wa wageni wanaocheza kwenye nafasi zao.

Ni vigumu kumuweka nje Tambwe na Ngoma wakiwa kwenye ubora wao, ili washambuli hawa wa kizalendo wapate nafasi kwenye kikosi cha Yanga wanatakiwa kufanya kazi ya ziada, kujituma uwanjani na kutekeleza maelekezo ya kocha ili kumfanya awaamini na kuwapa nafasi.

Ligi imemalizika, wachezaji wazawa mmejifunza nini kutoka kwa wageni ili kujipanga kwa ajili ya changamoto za msimu ujao? Au mnasubiri tena kuja kuwekwa benchi na kuwaangalia wageni wakishine huku nyinyi mkiishia kushikilia viatu mkononi na mechi zenu kubaki kwenye mazoezi?