WAKUU wa nchi za Afrika wametaka kuwepo na juhudi za pamoja katika kukabiliana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabiachi yanayolikumba bara hilo.
Kauli hiyo ilitolewa jana mchana (Jumanne, Mei 24, 2016) wakati wa majadiliano baina ya viongozi kutoka Zambia, Chad, Nigeria, Msumbiji na Tanzania mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 51 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano cha kimataifa wa Mulungushi, jijini Lusaka, Zambia.
Wakishiriki kwenye mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliohusu Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi, viongozi hao walisema bara la Afrika linahitaji kupata maendeleo zaidi licha ya tatizo la nishati linalolikumba bara hilo hivi sasa.
Akichangia mjadala huo, Rais wa Zambia, Bw. Edgar Lungu alisema nchi yake imepania kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme vijijini lakini imekuwa ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa mvua kwa zaidi ya miaka miwili hali ambayo alisema imechangia kukosekana kwa umeme katika maeneo mengi nchini humo.
“Uhaba wa mvua umepunguza kiwango cha maji katika bwawa la Kariba ambalo hutumika kuzalisha umeme nchini mwetu. Na hapa kwetu, karibu asilimia 80 ya umeme wetu, unategemea uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vya maji,” alisema.
Rais wa Chad, Bw. Idriss Deby Itno aliitaka benki ya AfDB ichukue nafasi ya mdau mkuu kwenye uwekezaji wa sekta ya nishati na kuzisadia nchi za bara hili kupata mitaji ya uwekezaji na ushauri wa kitaalamu.
“Tunahitaji kutumia fursa ambazo benki yetu inazo katika kukabilianana changamato za ukosefu wa nishati. Tukiweza kutekeleza jambo hilo, tutafanikiwa kuwa na miradi ambayo ni makini na kwa maana hiyo tutaweza kuliangaza bara letu la Afrika kwa kupata mwanga wa uhakika,” alisema.
Kwa upande wake, Makamiu wa Rais wa Nigeria, Prof, Yemi Osinbajo alisema bara la Afrika halina budi budi kuweka kipaumbele kwenye masuala ya maendeleo yake wakati likitafuta suluhisho la kukabiliana na athari za mazingira.
“Tunapaswa kutafuta njia za kubalance mahitaji makubwa ya umeme ambayo bara letu linakabiliwa nayo dhidi ya athari za kimazingira ambazo zinapigiwa kelele na mataifa makuna na zinahatarisha kutunyima fursa ya kuendelea haraka kama ilivyokuwa kwao,” alisema na kuongeza:
“Kama nchi zilizoendelea zinataka sana kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, zinatakiwa zitupatie fedha, teknolojia na wataalamu ambao watasaidia kuendesha mitambo ili tupate nishati safi kutokana na mafuta ya petroli na dizeli sababu ni rasilmali ambazo tunazo.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema ili kuondokana na tatizo la nishati, kuna haja ya kuwa na viongozi wenye utashi wa kisiasa ambao watakuwa tayari kuruhusu uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya nishati na kuongeza kuwa Tanzania inapitia upya sheria zake ili kuruhusu miradi mikubwa ya uwekezaji kwenye sekta hiyo.
Aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi kwa ajili ya wawekezaji walio tayari kuwekeza kwenye sekta hiyo na kutaja fursa ambazo Tanzania inazo kwenye sekta ya nishati ikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, madini ya urani, maji, upepo na nishati ya joto kutoka ardhini (geothermal energy).
Naye Waziri Mkuu wa Msumbiji, Bw. Carlos Agostinho do Rosário alisema kuna haja ya kuwa na taasisi ya uzalishaji na ugawaji umeme ya pamoja (electricity pool) ambayo itaruhusu wazalishaji wa umeme wawauzie wanunuzi wakubwa.
Waziri Mkuu ambaye yuko Lusaka kuhudhuria mkutano huo wa ADB kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, amerejea nchini leo (Jumatano, Mei 25, 2016).