Rais wa klabu ya Simba Evans Aveva (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu Simba kuboronga kwenye mashindandao ya msimu huu (VPL na FA Cup) kushoto ni Haji Manara-ofisa habari wa Simba
Na Baraka Mbolembole
Mwanzoni mwa wiki hii rais wa klabu ya Simba SC, Evance Aveva alikutana na wana habari na kuelezea matatizo makubwa zaidi manne ambayo yamechangia timu hiyo kushindwa katika matarajio yao ya kushinda taji lolote kati ya FA Cup na ligi kuu Tanzania bara inayotaraji kufunga msimu siku ya Jumapili hii. Aveva alitoa sababu nne (4)
Kwanza, ‘Wachezaji wameiangusha Simba, Pili, ‘Ushindani Mkubwa katika ligi, Tatu, ‘ Utendaji mbovu wa TFF’ Nne, ‘Waamuzi.’
Hotuba yake mimi naweza kuiandika kwa dakika kumi tu. Nimekuwa kimya lakini si kwamba siwezi kuijibu. Asilimia fulani ya wana Simba hivi sasa wanaamini na kufahamu matatizo yaliyoiangusha timu yao kwa mara nyingine msimu huu.
Lakini kinachonisikitisha ni taarifa yenyewe ambayo licha ya ufupi wake, haikubeba matarajio yaliyopita wala mapya klabuni hapo. Nini kazi ya Haji Manara? Kama mkuu wa kitengo cha habari wa klabu hiyo ameshindwa vipi kuhakikisha taarifa ambayo rais wa klabu angeisoma kwa maana ya kuwaelewesha wanachama na mashabiki wao?
Hii Simba ni ‘pasua kichwa’. Mfano, katika sababu yao ya kwanza, wachezaji kuiangusha timu. Ingawa hawakutaja majina ya wachezaji lakini maelezo yao yamelenga matukio ya mlinzi Hassan Kessy (kupiga pasi ya kurudi nyuma kwa golikipa lakini mshambulizi, Donald Ngoma akaiwahi na kuifungia Yanga goli la kuongoza Februar 20 katika mechi ambayo Simba walipoteza 2-0.
Pia walimaanisha tukio la Kessy kulambwa kadi nyekundu dakika chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili katika mechi waliyopoteza 1-0 dhidi ya Toto Africans katika uwanja wa Taifa. Kessy aliondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumrukia Edward Christopher.
Katika sababu hii ya kwanza iliyotajwa na Aveva, upande wangu namtaja Haji Manara. Niliwahi kuandika kuwa, Manara ameshindwa ndani ya uwanja, akashindwa nje ya uwanja na angeshindwa mahakamani alipotaka kwenda kuzuia Simba isiandikwe kwa mabaya.
Alikuwa mtu wa kutapatapa kwenda katika kituo fulani cha radio na kutishiatishia watu. Ajabu eti, wenyewe sasa wanasema radio hiyo imechangia kuanguka kwao. Mtazamo finyu kabisa. Manara ameingusha Simba kwa kuwa alikuwa akishinikiza TFF ifanye wanachotaka.
Mfano kukataa kuendelea kucheza mechi zao, wakati timu ilikuwa fomu na wapinzani wao walikuwa wakiwahofia. Mechi walizogomea kucheza eti hadi Yanga SC na Azam wamalize viporo vyao zote Simba walipaswa kucheza uwanja wa Taifa. Simba ingecheza game zile ingeshinda dhidi ya Toto na Mwadui FC-Jumlisha pointi 6 katika hizi 62 walizonazo!
Masikini, Manara hajui atendalo alafu yeye ndiye mkuu wa kitengo cha habari klabuni. ‘Simba si ya baba yako’ tafakari kauli zako braza, mchezaji hatukanwi na kiongozi wake, hata kwa siri. Manara ni sababu ya kwanza muhimu kuanguka kwa Simba, ‘aliisimamisha timu iliyokuwa katika mwendo kasi, huku ikianza kuogopeka.’ Msiwasingizie wachezaji tafadhali, hapa mchawi ni Manara.
Simba imeshinda game 19 kati ya 29 walizokwisha cheza. Ni timu ya pili iliyoshinda michezo mingi msimu huu nyuma ya mabingwa Yanga waliofanikiwa kushinda game 22-mechi 3 zaidi ya Simba. Sababu yao ya pili kuangushwa na ushindani haina mashiko.
Nachokiona labda wangetaja utulivu ndani ya timu yao kwa maana timu inapokosa umoja si rahisi kupata matokeo mazuri hasa inapotokea utengano huo ndani ya wachezaji wenyewe. Nidhamu ya timu kiujumla imewaangusha Simba hili linapaswa kutazamwa pia.
Sare tano na vipigo vitano vimetosha kuwanyima Simba taji la VPL msimu huu. Kwa sababu Manara hafahamu kutazama mpira na kujua sababu za kuanguka kwa timu yao aende kwa Jerry Murro pale Yanga akapate ujuzi wa kuzungumza na pengine hata kuandika taarifa nzuri ambayo rais wa klabu ataiweka wazi kwa wanachama.
Ligi yoyote ile kikawaida huwa ina ushindani, inategemea timu husika inashindania nini.
Sababu yao ya Tatu kuhusu utendaji mbovu wa TFF ina mashiko ndani yake. Kwa maana waamuzi wamekuwa tatizo na mpangilio wa ratiba umekuwa ukibadilika badilika mara kwa mara wakati ligi ikiendelea. Nafikiri, hapa wangejiweka na wao pia.
Wangesema, ‘Utendaji wetu viongozi wa Simba na udhaifu uliopo TFF na bodi ya ligi umetuangusha.’ Wangeeleweka, ila kuitaja TFF pekee huku wao wakiacha hata kujigusa ni ‘upuuzi’ ambao wana Simba hawatapenda kuusikia.
Kuna wakati namuhurumia Aveva kwa mzigo mkubwa aliojitwisha, lakini acha aendelee kutaabika kwa maana amekosa meno wala sauti ya maamuzi kama rais wa klabu. Mtu mmoja anayumbisha timu nzima ya utawala hadi ndani ya uwanja, na anaendelea kuhusudiwa naye.
Aveva ungemtaja Hans Poppe badala ya TFF na kueleza sababu, ungeeleweka. Labda kama ulisoma kitu ambacho hukikielewa. Sababu muhimu za kufanya vibaya kwa Simba, hatajwi Poppe na kutajwa TFF! Simba inakwenda wapi sasa? Sababu yao ya 3 haina mashiko, ila kwa TFF ujumbe umefika, vipi kwa Poppe?
Sababu ya nne kuhusu waamuzi ina mashiko na si Simba tu waliothiriwa na uchezeshaji mbovu wa baadhi ya waamuzi bali hata mabingwa Yanga, Azam FC, Coastal Union, Toto na timu nyinginezo zote zimeangushwa pia na waamuzi.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata updates za michuano mbalimbali. Asanteni.