SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 6 Aprili 2016

T media news

Ushirikiano zaidi wa Ufaransa na Afrika katika kupambana na ugaidi


Ushirikiano zaidi wa Ufaransa na Afrika katika kupambana na ugaidi
Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesisitiza kuwa, Ufaransa na Afrika zinapaswa kuwa na ushirikiano na uratibu zaidi katika kupambana na ugaidi.
Rais Hollande amesema hayo katika mkutano na waandish wa habari akiwa na mgeni wake Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye alikuwa Paris katika safari rasmi ya kikazi lengo likiwa ni kuimarisha na kupanua ushirikiano wa kiuchumi wa nchi mbili hizo. Rais wa Ufaransa aliashiria mashambulio ya kigaidi na ya kinyama ya mwaka 2013 na 2015 nchini Kenya pamoja na mashambulio ya kigaidi ya Paris yaliyotokea mwaka jana na kusema kuwa, nchi mbili hizo zinapaswa kuwa na ushirikiano zaidi katika suala zima la kupambana na ugaidi. Rais wa Ufaransa ameongeza kuwa, hata kama mashambulio ya kigaidi ya Kenya na Ufaransa hayakufanywa na kundi moja, lakini linalopaswa kufahamika ni kuwa, magaidi hao wametekeleza mashambulio hayo kutoka chimbuko fulani na irada ya makundi yote mawili ni moja nayo ni kutoa pigo kwa mwenendo wa maisha. Rais Hollande ameashiria kufungamana Ulaya na ahadi zake huko Somalia kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kusema kwamba, nchi yake na Ulaya zitafanya hima zaidi katika vita dhidi ya ugaidi barani Afrika.
Katika uwanja huo, Rais wa Ufaransa amesisitiza juu ya udharura wa kubadilishana taarifa zinazohusiana na watu au makundi ya kigaidi na kuongeza kuwa, kuna haja kwa pande husika kupeana tajiriba katika uga wa kupambana na vijana kuwa na misimamo ya kupindukia na kuwaondoa vijana hao katika hali hiyo.
Matamshi ya Rais wa Ufaransa yanatolewa katika hali ambayo, nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa kwa miaka mingi zimekuwa na ushawishi katika nchi mbalimbali barani Afrika. Filihali wanajeshi wa Ufaransa wapo katika akthari ya nchi za Kiafrika ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mali, uwepo ambao si tu kwamba, haujasaidia kuboresha hali ya mambo katika nchi hizo, bali vitendo vya wanajeshi hao vya ubakaji na kuwanajisi vijana wadogo vimeibua makelele na fedheha kubwa kimataifa. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, muamala wa sasa wa Ufaransa na uwepo wake katika nchi mbalimbali za bara hilo chimbuko lake ni kulinda maslahi yake makubwa barani humo.
Kwa sasa Ufaransa inakabiliwa na matatizo mengi ya ndani na nje. Suala la wahajiri, hitilafu zake na Umoja wa Ulaya, kudorora uchumi, ukosefu wa ajira na shambulio la kigaidi la Januari mwaka huu, ni mambo ambayo yameifanya nchi hiyo ifikirie kuwa na uwepo katika nchi nyingine hususan katika nchi za Kiafrika.
Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana suala la ugaidi na vita dhidi ya ugaidi kimekuwa ni kisingizio kizuri mno kwa wanasiasa wa Ufaransa ambapo katika kalibu ya kusaidia vita dhidi ya ugaidi waweze kupanua wigo wa harakati za nchi hiyo pamoja na satuwa na upenyaji wake katika nchi za bara hilo.
Matamshi ya Rais Francois Hollande nayo pia yametolewa katika uwanja huo na katika kuhalalisha uwepo wa nchi yake barani Afrika na vile vile kutaka kuwa na satuwa na nafasi zaidi barani humo.