SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 6 Aprili 2016

T media news

FAIDA ZA MACHUNGWA

                                                                                Faida Za Machungwa




Machungwa ni matunda maarufu sana sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania. Ni jamii ya matunda aina ya citrus, na yanapatikana kwa wingi na urahisi sehemu mbalimbali hapa nchini. Jamii hii ya matunda inajumuisha machungwa, machenza, tangarine, klementine  n.k.
Virutubisho Vinavyopatikana Kwenye Machungwa.
Machungwa yana mkusanyiko wa virutubisho vingi; Wanga, Protini kwa kiasi kidogo, Vitamini (A, B1,B2,B3,B5,B6,B9, C, E) madini (Kalsiam,Chuma, Zinki,Potasiam) na kambakamba (roughage/fibers).
Machungwa ni chanzo kikubwa na kizuri cha Vitamini C katika mlo. Chungwa la ukubwa wa wastani lina miligramu 50 za Vitamini C, na kwa kawaida mahitaji kwa siku ya Vitamini C ni miligramu 90 kwa mwanaume na miligramu 75 kwa mwanamke. Hivyo chungwa moja au mawili kwa siku yanaweza kutosheleza mahitaji hayo.
machungwa na juisi ya chungwa
machungwa na juisi ya chungwa
Machungwa yanaweza kuliwa kama tunda zima au kwa kunywa juisi ya machungwa. Juisi ya machungwa huwa na virutubisho vyote vya machungwa isipokuwa kambakamba (roughage/fibers), ambazo zipo kwa wingi zaidi  mtu napokula chungwa zima.
Nile machungwa mangapi kwa siku?
Inashauriwa kula chungwa moja au mawili kwa siku, kwani hii hutosheleza mahitaji ya Vitamin C na madini mengine mwilini. Ulaji wa machungwa mengi sana(zaidi ya 50) kwa siku unaweza kusababisha kujaa Vitamini C (hypervitaminosis) ambako ni hatari kwa afya.
Faida za Machungwa:

  • Huimarisha Kinga ya Mwili.
Vitamini C pamoja na madini mengine ikiwemo Zinki, yanatumika kwenye ufanyaji kazi wa mfumo wa kinga ya mwili.
  • Hupunguza Hatari ya Magonjwa ya Moyo na Saratani.
Machungwa yana kampaundi ziitwazo phytochemicals kama hesperedin, ambazo hulinda mishipa ya damu na kupunguza lehemu (cholesterol) kwenye damu.Vitamini C pia iliyopo kwenye machungwa huondoa sumu za mwili (free radicals), ambazo huchangia kutokea kwa saratani na magonjwa ya moyo zinapokuwa zimelundikana mwilini.
  • Huimarisha afya ya fizi na mdomo.
Vitamini C husaidia kujenga protini za kolajeni za fizi za mdomoni, hii huimarisha afya ya fizi. Ukosefu wa Vitamini C mara nyingi huambatana na fizi kuvuja damu kutokana na kukosa protini za kolajeni za kutosha.
  • Hupunguza lehemu(cholesterol) mwilini.
Machungwa yana kambakamba laini (soluble fibers) ambazo huyeyuka kwenye chakula. Hizi husaidia kunyonya mafuta ya lehemu(cholesterol) yaliyo kwenye chakula na kutolewa nje ya mwili kama choo. Hii hupunguza mafuta ya lehemu(cholesterol) kwenye mwili wa mtu.
  • Kuona vizuri.
Machungwa yana Vitamini A ambayao inasaidia kuhakikisha macho yanaona vizuri, pamoja na kamapundi nyingine ambazo hulinda tishu za macho zisiharibiwe na mwanga.
  • Hupunguza hatari ya kukosa choo/kupata choo kigumu (constipation).
Machungwa hasa pale mtu anapokula chungwa zima, humpatia kambakamba ambazo husaidia kulainisha chakula kwenye utumbo na kukifanya choo kuwa laini.
  • Huimarisha afya ya ngozi.
Madini yaliyopo kwenye machungwa pamoja na Vitamini A na C husaidia kujenga na kuondoa seli za ngozi zilizokufa.
Fanya machungwa kuwa sehemu ya mlo wako kila siku ufaidike na kazi zake.