SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 22 Machi 2016

T media news

Tanzania yatakiwa iendeleze mazungumzo Zanzibar


Tanzania yatakiwa iendeleze mazungumzo Zanzibar
Jamii ya Kimataifa imetoa wito wa kuendelea kutafutwa ufumbuzi wa kisiasa Zanzibar licha ya kurudiwa uchaguzi mkuu katika visiwa hivyo ambavyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Wanadiplomasia wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya (EU) pamoja na Marekani walioko nchini Tanzania wametoa taarifa ya pamoja mjini Dar es Salaam hapo jana mara baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani Zanzibar na kueleza kusikitishwa kwao na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuitisha uchaguzi wa marudio bila ya kufikiwa suluhisho la mgogoro wa kisiasa uliovikumba visiwa hivyo.
"Ili uwe na itibari, lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na kuakisi matakwa ya kweli ya wananchi", imeeleza taarifa ya mabalozi hao.
Taarifa hiyo imerudia tena wito wa nchi hizo wa kuitaka serikali ya Tanzania ichukue hatua ya kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo kwa kushirikisha vyama vikuu vya siasa ili kuweza kudumisha amani na umoja nchini humo.
Uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar ulifanyika siku ya Jumapili baada ya tume ya uchaguzi kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana kwa madai kuwa uligubikwa na vitendo vingi vya ukiukaji taratibu za uchaguzi.
Katika uchaguzi wa Jumapili, na kama ilivyotarajiwa, chama tawala CCM kimeibuka mshindi ambapo Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC imemtangaza mgombea wa kiti cha rais kupitia chama hicho, Dakta Ali Muhammed Shein mshindi wa uchaguzi huo.
Chama kikuu cha upinzani cha CUF kilisusia uchaguzi huo kwa madai kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 haukuwa na kasoro zozote na kwamba mgombea wake wa urais Maalim Seif Sharif Hamad alipasa kutangazwa mshindi wa uchaguzi. Madai hayo ya CUF yameungwa mkono na waangalizi wote wa uchaguzi huo wakiwemo wa ndani, wa kieneo na kimataifa.../