SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 6 Machi 2016

T media news

SIMBA YAITUNGUA MBEYA CITY KWA MARA YA KWANZA TAIFA NA KUREJEA KILELENI MWA VPL


Wachezaji wa Simba Awadh Juma (ushoto) na Ibrahim Ajib (kulia) wakishangilia goli la kwanza lilifungwa na Danny Lyanga
Ushindi wa magoli 2-0 iliyoupata leo timu ya Simba SC dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa taifa ni ushindi wa kwanza wa ‘Wekundu hao wa Msimbazi dhidi ya Mbeya Mbeya City kwenye uwanja wa taifa.

Simba ilikuwa haijawahi kuifunga City kwenye uwanja wa taifa tangu timu hiyo ilivyopanda kucheza ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara. Mechi ya kwanza Simba ilitoka sare ya kufungana kwa bao 2-2 dhidi ya Mbeya City kisha ikakubali kichapo cha goli 2-1 kwenye mchezo wa pili kabla ya leo kuikandamiza kwa mabao 2-0.

Magoli ya Simba kwenye mchezo wa leo yamefungwa na Danny Lyanga ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa kiganda Hamisi Kiiza kisha Ibrahim Ajib akatupia bao la pili baada ya kuongezwa dakika moja zikiwa dakika 90 zimemalizika.

Rekodi na matukio muhimu unayotakiwa kujua

Simba inafanikiwa kurejea kileleni mwa VPL kwa mara pili msimu huu

Simba inapanda kileleni mwa ligi kwa mara ya pili msimu huu baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza ilipoifunga Stand United kwa bao 2-1 kwenye uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga na kufanikiwa kukaa kileleni kwa mara ya kwanza Febuary 13, 2016 tangu ifanye hivyo misimu mitatu iliyopita.

Hata hivyo Simba iko mbele kwa mchezo mmoja ikiwa imeshacheza michezo 21 na kufikisha pointi 48 wakati wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha ubingwa Yanga na Azam wao wamecheza mechi 20 wakifanikiwa kukusanya pointi 47 huku wakiwa na mchezo mmoja wa kiporo kwa kila timu.

Ubingwa wa VPL bado mweupe kwa timu tatu za juu

Simba, Yanga na Azam zote zinaweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu huu kutokana na idadi ya pointi ambazo zinazitofautisha timu hizo pamoja na tofauti ya michezo huku idadi ya mechi zilizosalia ili ligi kumalizika ikipewa uzito wa wa juu kuamua nani atatwaa ubingwa msimu huu.

Simba imevunja mwiko wa kuteswa na Mbeya City kwenye uwanja wa taifa

Timu hizo tayari zimekutana mara tatu kwenye uwanja wa taifa huku Simba ikishindwa kutamalaki mara mbili mbele ya City, lakini leo imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza wa bao 2-0 na kuzima historia iliyokuwa imewekwa na wana-Mbeya hao.

Mbali na kushinda mchezo wa leo, Simba pia iliichapa Mbeya City kwenye mchezo wa round ya kwanza kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya hivyo kuchukua pointi zote 6 za msimu huu mbele ya Mbeya City.

Ushindi dhidi ya Mbeya City unamaana gani kwa Simba?

Baada ya kupoteza mechi yao dhidi ya Yanga, Simba inafanikiwa kushinda mbele ya Mbeya City na kupata matumaini makubwa ya kuwania ubingwa msimu huu tofauti na endapo wangepoteza mchezo au kutoka sare.

Simba sasa wanarejea kwa miguu yote kwenye kinyang’anyiro VPL baada ya kupunguzwa makali na Yanga walipokubali kichapo cha bao 2-0 na kuteremshwa kileleni mwa ligi hiyo ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya vilabu bingwa barani Afrika.

Nini kinafuata kwa timu hizo baada ya mchezo wa leo?

Simba itakuwa kwenyeji kwenye uwanja wa taifa ikiikaribisha Ndanda FC ya Mtwara March 10 mwaka huu wakati wakali wa Halmashauri ya jiji la Mbeya, Mbeya City wenyewe pia wataialika Coastal Union kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.