SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 26 Februari 2018

T media news

Waliomkimbia Waziri Alipofanya Ziara ya Kushtukiza Watakiwa Kujisalimisha Polisi Saa 10

Baada ya viongozi wa Kampuni ya  Ujenzi ya Jesco ya jijini Mwanza kumkacha ‘kiana’ alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za kampuni hiyo, Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amewaamuru kuripoti ofisini kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza kabla au ifikapo saa 10:00 jioni leo..

Mavunde ametoa agizo hilo leo Februari 26 baada ya kuwasubiri viongozi hao ofisini kwao kwa zaidi ya saa nzima bila mafanikio.

Pamoja nao, naibu waziri pia ameuagiza uongozi wa kampuni hiyo kuwasalimisha kwenye mamlaka husika wafanyakazi wawili raia wa kigeni walioajiriwa kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari na wafanyakazi wa ngazi ya chini aliowakuta eneo la ofisi hizo alipofanya ziara ya kushtukiza, Mavunde amesema uongozi wa kampuni hiyo unatuhumiwa kutowalipa mishahara wafanyakazi kwa muda mrefu pamoja na kuajiri raia wa kigeni bila kufuata taratibu za kisheria.

“Kosa lingine ni kutojisajili kwenye mfuko wa wafanyakazi (CWF), licha wizara kutoa maagizo ya kufanya hivyo mwaka mmoja uliopita,” amesema Mavunde.

Amesema iwapo tuhuma dhidi ya uongozi huo zitathibitishwa, wahusika wanakabiliwa na hatari ya kufingo cha miaka sita jela au faini ya Sh50 milioni au adhabu zote kwa pamoja.

Baada ya kutoa maagizo hayo, Mavunde ameamua kuondoka katika ofisi za kampuni hiyo kuendelea na ziara katika maeneo mengine.

Awali, baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na naibu waziri wakiomba kutotajwa majina gazetini wamesema mkurugenzi na meneja uajiri wa kampuni hiyo wameamua kuingia mitini kukwepa kujibu tuhuma dhidi yao za kutowalipa mishahara wafanyakazi kwa muda mrefu.

“Inawezekana taarifa za ziara ya kushtukiza ya waziri zimevuja ndio maana wamekimbia,” amesema mmoja wa wafanyakazi hao

Akizungumzia ziara yake ofisini hapo, Mavunde amesema imetokana na taarifa za siri alizopata kuhusu ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za kazi ikiwemo kutowalipa wafanyakazi mishahara, ajira kwa wageni kinyume cha sheria na kutojisajili CWF.