SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 31 Desemba 2016

T media news

Tanzania yapaa kiuchumi kusini mwa Jangwa la Sahara

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Tanzania imebaki kuwa miongoni mwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara Barani Afrika, ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Dk Mpango alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2016 na matarajio hadi Juni, 2017.

Alisema ukuaji wa uchumi ni mojawapo ya vitu vinavyotazamwa katika kutathmini afya ya uchumi wa taifa.

Akifafanua, alitoa mfano kwa baadhi ya nchi hizo kuwa mwaka jana Tanzania uchumi wake ulikuwa kwa asilimia 7.0 na mwaka huu unakua asilimia 7.2, Kenya mwaka jana ulikua asilimia 5.6 na mwaka huu unakua asilimia 6.0, Uganda mwaka jana ulikuwa asilimia 4.8 na mwaka huu unakuwa asilimia 4.9.

“Kwa mifano hiyo tunaona Tanzania imeendelea kufanya vizuri uchumi unakuwa kwa kasi kubwa katika Bara la Afrika,” alisema.

Kwa upande mwingine, alisema kuwa ustawi wa uchumi wa taifa unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali vikiwemo ukuaji wa pato la taifa, mfumko wa bei, thamani ya shilingi, mwenendo wa sekta ya kibenki na sekta ya nje na akiba ya fedha za kigeni.

Akizungumzia mfumuko wa bei, alisema ulipungua kutoka asilimia 6.5 Januari 2016 hadi asilimia 5.5 Juni 2016 na kupungua zaidi hadi asilimia 4.5 Septemba mwaka huu. Baadaye ulipanda kidogo mwezi Novemba na kufikia asilimia 4.8.

“Maana yake ni kuwa bei za bidhaa na huduma ziliongezeka kwa kasi ndogo zaidi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. Mwenendo huu wa kushuka kwa mfumuko ulichangiwa na kasi ndogo ya ongezeko la bei za chakula nchini, kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na fedha na utulivu wa thamani ya shilingi. Kupanda kwa mfumuko wa bei mwezi Novemba kulitokana na kupungua kwa upatikanaji wa bidhaa za chakula pamoja na mkaa,” alisema.

Alisema thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika dhidi ya dola ya Marekani. Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati ya shilingi 2,167 hadi 2,199 kwa dola moja ya Marekani.

“Hali hii ilitokana na kuwa na sera thabiti za uchumi pamoja na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha za kigeni hususan kutokana na mauzo ya bidhaa za viwandani, utalii na huduma mbalimbali,” alisema.

Akizungumzia mwenendo wa sekta ya kibenki alisema mabenki yetu ni imara na salama yakiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha.

Alisema amana za wateja katika mabenki zilipungua kidogo kutoka Sh trilioni 20.73 mwezi Disemba 2015 kufikia Sh trilioni 20.57 mwezi Septemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, sababu zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania.

Waziri huyo alisema kati ya Julai hadi Novemba mwaka huu, mikopo nafuu iliyopokelewa ni sh. bilioni 316.4 sawa na asilimia 17.6 ya lengo la Sh bilioni 1,793.7.

Alisema sababu ya kutofikiwa malengo ya upatikanaji wa misaada ya mikopo nafuu ni pamoja na masharti magumu yaliyowekwa na wahisani, hata hivyo serikali inatarajia kukamilisha majadiliano na AfDB kati ya Desemba mwaka huu hadi Machi, 2017.

“Aidha majadiliano na benki ya dunia na Umoja wa Ulaya, bado yanaendelea. Kuhusu fedha za miradi, jitihada zinafanyika katika sekta husika kukamilisha taarifa za miradi zinazohitajika na wafadhili,” alisema.

Dk Mpango alisema katika mwaka 2016/17, serikali ilipanga kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara kiasi cha dola za kimarekani milioni 936 sawa na Sh bilioni 2,100.9 ili kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hata hivyo, hadi kufikia Novemba, 2016 serikali haikukopa kutoka katika chanzo hiki kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016/17.

“Hali hii ilisababishwa na mdororo wa kiuchumi katika bara la Ulaya na hivyo kuongezeka kwa gharama za mikopo na kuathiri upatikanaji wake. Mfano, riba ilipanda kutoka wastani wa asilimia 6 hadi asilimia 9. Kutokana na sababu hiyo, serikali iliahirisha kuendelea na mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko hayo na badala yake ikajielekeza kukopa kutoka nchi nyingine za China, India, Korea Kusini na Japani,” alisema Dk Mpango.

Kwa upande wa ulipaji wa madai mbalimbali, alisema katika kipindi cha Julai hadi Novemba, mwaka huu madai yaliyohakikiwa ya jumla ya Sh bilioni 318.556 yalilipwa, ambapo Sh. bilioni 183.714 ni kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi washauri wa miradi ya barabara.

Fedha nyingine Sh bilioni 42.951 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji, Sh bilioni 30 kwa ajili ya mikataba ya ulinzi na usalama, shilingi bilioni 25 kwa ajili ya miradi ya umeme, Sh bilioni 15.439 kwa ajili ya wazabuni mbalimbali, Sh bilioni 10 kwa ajili ya madai ya watumishi, Sh bilioni 7 kwa ajili ya matibabu nje ya nchi kama hospitali ya Apollo, India, Sh bilioni 3.150 kwa ajili ya mtaalamu mwelekezi wa mipango miji ya jiji la Arusha na Mwanza, Sh bilioni 1.302 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali ya serikali.

Alisema deni la taifa limeendelea kuongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 21,087.9 mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, kutoka dola za Marekani milioni 19,861.1 Disemba mwaka jana. Deni la ndani liliongezeka kufikia sh. bilioni 10,089.3 mwishoni mwa Oktoba mwaka huu kutoka sh. bilioni 8,597.0 Desemba mwaka jana.