Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) chini ya Rais wake, Chaulembo Palasa imemfungia kwa miaka miwili bondia Francis Cheka ‘SMG’ kushiriki mchezo huo pia imempiga faini ya Sh 500,000 adhabu ambazo Cheka amegoma kuzitambua
TPBC imemfungia Cheka baada ya kugomea pambano lake dhidi ya Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ ambalo lilipangwa kufanyika Desemba 25, mwaka huu kwenye Ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam.
Katibu Msaidizi wa TPBC, Michael Chatta amesema kamati ya utendaji iliyokaa Desemba 27, mwaka huu imeamua kumfungia Cheka baada ya kukutwa na makosa ya kimakubaliano na promota wake.
Chatta alisema kamisheni hiyo ilipokea mkataba wa promota Kaike ukimhusisha Cheka kwa ajili ya pambano lake dhidi Dullah Mbabe huku kukiwa na makubaliano ya kimkataba kwamba anatakiwa kulipwa sh. milioni tatu za awali na shilingi milioni sita baada ya pambano hilo lakini hata hivyo bondia huyo aligomea.
“Kamisheni tumeamua kuchukua hatua ya kumfungia Cheka baada ya kujiridhisha kwamba amechukua fedha pasipo kuifanya kazi aliyotakiwa kuifanya, kitu ambacho hakiwezi kukubalika.
Chaurembo Palasa
“Kitendo hicho kinapoteza uaminifu, kuwakimbiza wadhamini pamoja na kuleta uvunjifu wa amani. Lakini kwa mujibu wa sheria ya ngumi za kulipwa Tanzania kupitia kifungu cha nne, kifungu kidogo cha kwanza, Cheka amekutwa na makosa, hivyo amefungiwa kushiriki kwa namna yoyote mchezo wa ngumi kwa muda wa miaka miwili pamoja na kulipa faini ya Sh laki tano,” alisema Chatta.
Alipotafutwa Cheka na kutakiwa kuizungumzia adhabu hiyo, alisema: “Hao wananifungia kwa lipi? Mimi siyo mwanachama wao halafu nimeshastaafu, sasa hii inatoka wapi, wanajua kwa nini nilikataa kucheza pambano lile?”
Francis Cheka
Kwa upande wake Cheka Mwenyewe amepiga maamuzi hayo ya TPBC na kudai wamepotoka kutangaza kumfungia na kimsingi hawana sifa na uwezo wa kumfungia yeye kwani yeye sio mwanachama wa TPBC na hata hivyo kama kweli walitaka haki basi wangemwita na yeye kwanza ili wamsikilize badala ya kusikiliza upande mmoja wa mlalamikaji.
Cheka pia alienda mbali zaidi na kutaka uchunguzi wa kipolisi ufanyike akidai kughushiwa kwa saini yake katika mkataba ambao umetumika kumwadhibu yeye jambo ambalo amesema kuna njama za wazi za kutaka kumchafua.