SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 23 Julai 2016

T media news

DEAL DONE: Pogba Avunja Rekodi ya Uhamisho wa Dunia


WAZUNGU wanasema kwa Kiingereza chao, Deal done. Yaani biashara imekwishamalizika. Watu wananyanyuka katika viti vyao, wanapeana mikono, wanakumbatiana, wanaondoka. Uhamisho wa Paul Pogba inasemekana umemalizika.

Manchester United imefanikiwa kumnasa kiungo huyo mahiri wa Juventus kwa dau la Pauni 100 milioni ambalo litaweka rekodi mpya ya uhamisho duniani na kulipiku dau la Pauni 85 milioni ambalo Real Madrid walilipa mwaka 2013 kumchukua Gareth Bale kutoka Tottenham.

Licha ya kulipa dau hilo, United watamlipa Pogba mshahara wa pauni 210,000 kwa wiki kwa mkataba wa miaka mitano ikiwa ni miaka minne tangu alipomruhusu kuondoka bure kwenda Juventus Julai 2012 akiwa mchezaji kinda.

Bosi wa Man United, Ed Woodward alikacha kwenda katika ziara ya United nchini China na alikutana na Wakurugenzi wa Juventus, Giuseppe Marotta na Fabio Paratici, pamoja na wakala wa Pogba, Mino Raiola kwa ajili ya kumaliza dili hilo.

Juventus iling’ang’ania dau hilo licha ya Man United kujaribu kushusha, lakini mwishowe Man United imekubali kulipa dau hilo kwa staa huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye amezaliwa nchini Ufaransa na wazazi wake waliotokea Guinea barani Afrika.

Kocha wa Man United, Jose Mourinho alikuwa anamtaka staa huyo kabla ya pambano la ngao la hisani kati yao na Leicester City Agosti 7 na atajiunga nao mara baada ya timu hiyo kurejea katika ziara ya maandalizi ya msimu mpya nchini China ambako wametua juzi.

Pogba aliondoka Old Trafford katika utawala wa kocha mkongwe, Sir Alex Ferguson baada kushindwa kuhakikishiwa nafasi katika kikosi cha kwanza kilichokuwa kimesheheni mastaa wakongwe kama Paul Scholes ambaye Ferguson hakutaka kumuweka benchi na alimuamini zaidi.

Tangu hapo, Pogba ameibuka kuwa mmoja kati ya viungo bora barani Ulaya huku akiiwezesha Juventus kutwaa ubingwa wa Serie A mara nne, akiifikisha pia katika fainali za Ulaya pamoja na kuipeleka Ufaransa katika fainali za Euro 2016 ambapo walichapwa 1-0 na Ureno.

Mfaransa huyo atakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Man United dhini ya Mourinho baada ya kuwanasa Eric Bailly kutoka Villarreal, Zlatan Ibrahimovic aliyenaswa bure kutoka PSG na Henrikh Mhkitaryan aliyechukuliwa kutoka Borussia Dortmund.

Wakati dau la Pogba likianza kulalamikiwa na wadau wengi wa soka kwamba haliendani na kiwango chake, tayari nyota huyo ameanza kupata watetezi akiwemo staa wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry.

“Sahau kuhusu Ufaransa, nadhani anaweza kuwa mmoja kati ya viungo bora katika historia. Ana ubora wa kufanya hivyo. Anahitaji kuwa makini tu na kitu anachoweza kukifanya vizuri.” Alisema Henry katika michuano ya Euro.