Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Lindi imekifunga Kiwanda cha Saruji cha Kilwa kinachomilikiwa na Kampuni ya Lee Bulding Material Limited kwa madai ya kushindwa kulipa kodi ya Sh89 milioni.
Hata hivyo, mwakilishi wa kampuni hiyo, Ismail Ali alikiri kuwapo kwa deni hilo, akidai kuwa kiwanda kilisimama kwa miezi mitano kutokana na kukosa malighafi hali iliyosababisha wamiliki kuzifuata nje ya nchi.
Meneja wa TRA Mkoa wa Lindi, John Jofrey alisema wafanyabiashara hao wamekaidi agizo la Serikali la kutakiwa kulipa kodi ya mali, ukaguzi zuio, vat na uendelezaji ufundi stadi.
“Tumewapa maagizo, tumewahamasisha lakini bado wamekaidi agizo letu, uamuzi tuliochukua ni kufunga kiwanda kupitia wakala,” alisema Jofrey.
Alisema lengo la kufikia hatua hiyo ni kuhimiza wafanyabiashara kulipa kodi stahiki kwa wakati badala ya kusukumana.
Dalali wa TRA kutoka Mchinga Auction, Doment Likome alisema wamepata idhini ya kuzuia mali za kiwanda hicho hadi watakapo lipa deni hilo kwa muda wa siku saba.
Alisema wakishindwa kulipa, mali zilizopo kiwandani zitapigwa mnada.