SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 5 Novemba 2017

T media news

Simba inahitaji Ushindi Kuliko kitu Chochote Kulinda Heshima

Mchezo kati ya Mbeya City dhidi ya Simba unasubiriwa kwa shauku kubwa na wadau wa soka nchini kwa sababu ni mchezo utakaoamua kinara wa ligi kuu Tanzania bara baada ya mechi za mwisho wa juma hili.

Simba inahitaji ushindi kuliko kitu chochote kwenye mchezo huo ili kuendelea kuongoza ligi hasa baada ya matokeo ya mechi za jana (Jumamosi November 4, 2017) ambapo wapinzani wa Simba kwenye nafasi ya kwanza Yanga na Mtibwa zilibanwa na kulazimishwa sare huku Azam ikishinda na kuongoza ligi baada ya kufikisha pointi 19 pointi mbili zaidi ya Yanga na Mtibwa ambazo zilicheza jana.

Pointi tatu pekee ndio zitaifanya Simba kurejea kwenye nafasi yake, matokeo tofauti na hayo maana yake ‘Mnyama’ atapoteza uongozi wa ligi kwa kuiacha Azam itawale kileleni. Endapo Simba itashinda itafikisha pointi 19 sawa na Azam lakini wastani mzuri wa magoli utaipeleka kwenye nafasi ya kwanza, matokeo ya sare yoyote yataifanya ibaki nafasi ya pili kwa wastani wa magoli kwa sababu  italingana pointi na Mtibwa pamoja na Yanga. Ikipoteza mbele ya City itaendelea kusalia katika nafasi ya nne ambayo ipo sasa ikiwa na pointi 16.

Matokeo ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya

Wameshinda mechi tatu kati ya nne walizocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani, hawajashinda mechi yoyote nje ya Mbeya matokeo yao ya ushindi yamepatikana kwenye uwanja wa Sokoine. Mbeya City tayari imecheza mechi nane, imeshinda michezo mitatu, sare mbili huku ikiwa imepoteza michezo mitatu.

‘Wana-koma kumwanya’ wamepoteza mchezo mmoja wakiwa uwanja wa Sokoine huku mechi nyingine mbili wakidondosha pointi sita kwenye viwanja vya ugenini.

Mbeya City 1-0 Majimaji
Mbeya City 0-1 Ndanda
Mbeya City 1-0 Njombe Mji
Mbeya City 2-0 Ruvu Shooting
Katika magoli tisa waliyofunga kwenye mechi zao nane, manne kati ya hayo wamefunga wakiwa kwenye uwanja wa Sokoine na magoli matano yakifungwa kwenye viwanja vya ugenini.

Matokeo ya mechi za Simba nje ya uwanja wa Uhuru

Simba hawana rekodi nzuri wanapocheza viwanja vya ugenini, wameshinda mechi mmoja kati ya tatu walizocheza nje ya uwanja wa Uhuru. Ushindi pekee wa Simba katika mechi walizocheza nje ya uwanja wa Uhuru ni dhidi ya Stand United ya Shinyanga. Mchezo wa Yanga vs Simba haujahesabiwa kama wa ugenini kwa sababu uwanja huo ni wa nyumbani kwa vilabu vyote viwili kinachobalika ni zamu ya timu ipi kuwa nyumbani na nyingine kuwa ugenini kwenye uwanja huohuo.

Azam 0-0 Simba
Mbao 2-2 Simba
Stand United 1-2 Simba
Simba imefunga magoli manne tu nje ya uwanja wa uhuru kati ya magoli 20 iliyofunga katika mechi nane zilizopita za ligi kuu.

Matokeo ya Mbeya City vs Simba uwanja wa Sokoine, Mbeya

Mbeya City imecheza mara nane (mechi zote nyumbani na ugenini) mechi za VPL dhidi ya Simba tangu timu hiyo ya jijini Mbeya ilipopanda kucheza ligi kuu Tanzania bara msimu wa 2013/2014. Katika mechi nne ambazo Mbeya City imekutana na Simba kwenye uwanja wa Sokoine, Simba imeshinda mara mbili, imefungwa mara moja na kuambulia sare mara moja.

12/10/2016 Mbeya City 0-2 Simba
17/10/2015 Mbeya City 0-1 Simba
18/04/2015 Mbeya City 2-0 Simba
15/02/2014 Mbeya City 1-1 Simba