Serikali imesema itaongeza mishahara ya watumishi wake mwishoni mwa mwezi huu, sambamba na kuwapandisha madaraja kuanzia mwezi huu pia.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, ndiye aliyetangaza neema hiyo kwa watumishi jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akieleza mafaniko ya serikali ya awamu ya tano kwa kipindi chake cha miaka miwili.
Dk. Abbasi alisema mwishoni mwa mwezi huu, serikali itawaongeza mishahara watumishi wake pamoja na kuwapandisha madaraja.
"Mwezi huu tutawaongezea mishahara wafanyakazi na watumishi wa serikali watapanda madaraja na watalipwa stahiki zao," alisema Dk. Abbasi.
Kupandishwa mishahara na madaraja kwa watumishi wa umma kulisitishwa na serikali Machi mwaka jana ili kupisha uhakiki wa watumishi hewa na wafanyakazi wenye vyeti feki.
Oktoba 14, mwaka huu visiwani Zanzibar, wakati wa kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na maadhimisho ya miaka 18 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Rais John Magufuli alisema serikali yake itawapandisha vyeo na kurekebisha mishahara ya watumishi 59,967 baada ya kumalizika kwa uhakiki wa vyeti feki na watumishi hewa.
Rais Magufuli katika hotuba hiyo siku hiyo, alitolea mfano uzalendo wa Baba wa Taifa ambaye wakati wa uhai wake aliamua kupunguza mshahara wake na kukataa kuongeza mishahara ya watumishi wachache huku walio wengi wakipata shida.
“Ninaposema hivyo simaanishi kuwa mishahara isiongezwe. La hasha! Ninachosema ni kwamba kabla ya kudai nyongeza ya mishahara ni lazima kwanza kufahamu uwezo wa serikali, lakini pia tutambue kuwa kuna Watanzania wenzetu wengi tu wanaohitaji kuboreshewa huduma," alisema.
Rais Magufuli aliongeza: "Baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na vyeti feki, Serikali imewapandisha vyeo na kuwarekebishia mishahara watumishi 59,967 ambapo kiasi cha Sh. bilioni 159.33 zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu na mishahara mipya itaanza kulipwa kuanzia mwaka huu."