Abiria wa daladala inayofanya safari kati ya Gongo la Mboto na Makumbusho jijini Dar es Salaam, jana walikumbwa na taharuki baada ya basi hilo kuzimika katikati ya reli.
Hatua hiyo ilisababisha abiria hao kuruka kupitia madirishani ili kujinusuru huku treni ikiwakaribia.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya asubuhi, eneo la kituo maarufu kama Bakhresa, Buguruni, barabara ya Mandela na kuwafanya abiria kusukumana na baadhi wakigombea kupita katika mlango.
Chanzo cha kuaminika kilisema kuwa daladala hiyo yenye namba za usajili T 499 BGU na ubavuni namba S 108648 D ilizimika ghafla katikati ya reli huku kwa mbali wakiiona treni ya kutoka ubungo kwenda Stesheni katikati ya jiji, maarufu kama ‘treni ya ‘Mwakyembe’ ikikaribia eneo walilokwama.
“Abiria walikumbwa na taharuki huku wakiruka madirishani na wengine kugombea kupita mlangoni kujinusuru kugongwa na treni,” alisema mmoja wa abiria walionusurika.
Alisema kilichowasaidia kutopatwa na maafa ni kitendo cha dereva kusimamisha treni ili kupisha daladala hiyo kuondolewa katika njia yake.
Baadhi ya abiria waliokuwamo kwenye daladala hiyo, walisema tangu wakitoka Gongo la Mboto, ililonekana kuwa na matatizo na kwamba baada ya tukio hilo, abiria walioruka kwenye daladala hilo hawakurejea tena kupanda kwa kupatwa na hofu.