HATIMA ya ubomoaji wa nyumba ya kifahari ya Mchungaji wa kanisa la TAG Mikocheni, Getrude Rwakatare, inatarajiwa kuanza kujulikana leo wakati Naibu Waziri mpya wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola atakapotoa ripoti.
Wiki iliyopita Lugola aliomba Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kumpatia taarifa ya kukwama mwaka jana kwa ubomoaji wa 'hekalu' hilo lililopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Rais John Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri Oktoba 7 ambapo miongoni mwa sura mpya ni Naibu Waziri Lugola ambaye amechukua nafasi ya Luhaga Mpina aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
"Taarifa tayari ipo ofisini kwangu (tayari) nitaipitia Jumatatu (leo)," alisema Lugola ambaye alikuwa kwenye ziara mikoani wakati akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki. "Umma unataka kujua, hivyo siyo jambo la kucheleweshwa."
"Niliagiza nipatiwe taarifa ya tangu (sakata) ilivyoanza ili nijue ugumu (wa kubomoa) umetokana na nini halafu nitakwenda kushauriana na waziri wangu kile kilichojiri katika hiyo taarifa."
Mwanasheria wa NEMC, Heche Suguta alithibitisha kutekeleza agizo la naibu waziri kwa kuwasilisha taarifa ya jengo hilo liliopo kwenye viwanja namba 2019 na 2020 ofisini kwake.
"Siwezi kuzungumza chochote lakini alichokitaka waziri wangu tulitekeleze kabla ya muda aliotupatia," alisema Suguta ambaye pia alikuwa msimamizi mkuu wa bomoabomoa hiyo. "Tayari tumefanya hivyo."
Mchungaji Rwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) kwa kipindi cha pili, alihamia katika hekalu hilo Agosti 30, 2012 ambapo taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinasema waumini wa kanisa lake wapatao 300 walifika kushuhudia sherehe ya uzinduzi wa nyumba hiyo.
Nyumba hiyo ni moja kati ya 8,000 zilizokuwa zibomolewe mwishoni mwa mwaka 2015 katika operesheni maalum ya kuondoa makazi kwenye fukwe, kingo za mito, maeneo ya wazi na mabondeni.
Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Wakala wa Misitu (TFS) iliweka alama ya X kwenye kuta za nyumba hiyo wakidai imo katika hifadhi ya Bahari ya Hindi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, na kwamba pia imejengwa kwenye hifadhi ya mikoko.
Iliachwa baada ya mchungaji huyo kwenda mahakamani kufungua kesi ya kusimamisha zoezi hilo akipinga madai kuwa imejengwa ndani ya mita 60 kutoka fukwe ya bahari.
Aidha, mmiliki huyo alidai ujenzi wa nyumba hiyo ulishajadiliwa na kesi yake kuhukumiwa na Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi ambayo ilimuona Mch. Rwakatare hakuvunja taratibu zozote za ujenzi. Hukumu hiyo ilitolewa Mei 22, 2015.
Dk. Rwakatare, ambaye pia alikuwa mbunge wa viti maalumu kwenye Bunge lililopita, alipoteza nyumba nyingine nne zilizokuwa kwenye kiwanja namba 314 Mbezi Beach baada ya kubomolewa kwa tuhuma za kuvamia eneo hilo.