Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imeanza kulima majani aina ya lusini ambayo ni chakula cha Faru Fausta ili kupunguza gharama za kumtunza mnyama huyo.
Faru Fausta mwenye miaka 54 anahifadhiwa kwenye banda ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni hatua ya kumlinda asiliwe na wanyama wengine kutokana na jicho lake kutoona.
Amekuwa akitumia bandali 250 za majani kila baada ya miezi minne yanayoigharimu mamlaka hiyo Sh5 milioni. Majani hayo hununuliwa kutoka nchi jirani ya Kenya.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Idara ya Malisho na Usimamizi wa Wanyama NCAA, Hillary Mushi amesema mamlaka imeandaa shamba lenye ukubwa wa eka mbili na imepanda mbege za lusini. Amesema ndani ya miezi saba majani hayo yataanza kuvunwa.
Mushi amesema NCAA imechukua hatua hiyo ili kupunguza gharama za kumtunza faru huyo, ambaye amekuwa moja ya kivutio cha watalii na watafiti kutokana na kuwa ndiye faru mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani kati ya wanaoishi maeneo ya wazi hifadhini.
Akimzungumzia Faru Fausta, daktari wa wanyama katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Athanas Nyaki amesema ililazimika kumhifadhi kutokana na kuanza kushambuliwa na fisi.
Amesema kutokana na jicho la faru huyo kutoona na kukabiliwa na uoni hafifu katika jingine, alishambuliwa na fisi na kupata majeraha.
Dk Nyaki amesema tangu faru huyo amehifadhiwa afya yake imeimarika na majeraha yamepona.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni moja ya hifadhi chache nchini ambazo zina faru wengi, ambao wanalindwa kwa saa 24 kwa mitambo maalumu ili kuzuia wasiuawe na majangili.
Majangili wamekuwa wakiwaua faru ili kuchukua pembe zao ambazo huuzwa zaidi katika nchi za Mashariki ya Kati.