SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 10 Septemba 2017

T media news

Serikali Yataifisha Almasi ya Mabilioni Iliyokuwa Inatoroshwa Kwenda Ughaibuni

Almasi zenye uzito wa kilogramu 29.5 za thamani ya zaidi ya Sh bilioni 64, ambazo zilibakiza dakika tano tu kutoroshwa kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (JNIA) kwenda ughaibuni, zimetaifi shwa na serikali.

Aidha, watumishi wa serikali na maofisa wa Mgodi wa Almasi wa Williamson wa Mwadui Shinyanga, waliohusika na uthaminishaji wa awali wa almasi hizo na kudanganya kuwa zilikuwa na uzito wa kilogramu 14 tu, watachunguzwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akipokea ripoti ya timu ya wataalamu, iliyoundwa kuchunguza upya uzito na thamani halisi ya almasi hizo baada ya kuzikamata katika uwanja huo wa JNIA Agosti 31, mwaka huu.

Uthamini uliofanywa awali kwa almasi hiyo, iliyokuwa mbioni kupakiwa ndani ya ndege kutoroshewa nchini Ubelgiji, ulieleza kuwa ilikuwa na thamani ya chini ya Sh bilioni 32, huku ikielezwa pia kuwa na kilogramu 14, taarifa zilizogundulika kuwa zilikuwa ni za uongo.

Jana Waziri Mpango alipokea maelezo ya almasi hiyo kutoka kwa Kiongozi wa Jopo la Wataalamu waliofanya uthamini mpya, Profesa Abdulkarim Mruma na wasaidizi wake. 

Baada ya kuridhika na maelezo, yaliyodhihirisha kuwepo kwa kiwango cha juu cha udanganyifu kuhusu uzito na gharama za almasi hiyo, kwa lengo la kuliibia taifa, Waziri Mpango aliagiza almasi hiyo yote kutaifishwa, kupigwa mnada na fedha zitakazopatikana kuingia serikalini.

Aliagiza pia kuwajibishwa kwa maofisa wa serikali waliohusika katika udanganyifu huo kwa wahusika hao kukamatwa, kuchunguzwa mali zao ikiwemo majumba, mashamba, magari kuona kama vinaendana na mishahara yao na baadaye kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Alisema, Watanzania wamechoshwa kuona mali zao zikiibiwa kila kukicha huku serikali ikikosa mapato makubwa kutokea katika rasilimali hizo. 

Pia, aliagiza kuandaliwa kwa wataalamu wa madini na wapelekwe kwenye migodi haraka, kukabiliana na wizi wa aina hiyo, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na wizi wa aina hiyo.

Waziri Mpango aliagiza pia upimaji wa madini kufanyikia kwenye eneo la migodi, na pia kununuliwa kwa mashine za kupimia madini kwenye maeneo ya migodi, baada ya kuelezwa na Profesa Mruma kuwa ukosefu wa vifaa vya kupimia ni chanzo cha udanganyifu huo.

“Kazi nzuri sana umefanya Professa Mruma na wenzako na kwa sasa ninaagiza haya madini tuliyokamata hapa, kulindwa kuanzia hapa hadi pale yatakapoingizwa sokoni, pia ninamtaka Gavana wa Benki Kuu (Profesa Benno Ndulu) kuanza kuhifadhi madini ya vito na si fedha peke yake.

“Inashangaza kuona maofisa wa juu wa Wizara ya Nishati na Madini waliokuwa na jukumu la kuthaminisha madini haya wamedanganya huku wale walio chini yao wametoa tathmini ya kweli, sasa huu ndiyo uzalendo unaotakiwa,” aliongeza Dk Mpango.

Kwa upande wa Mgodi wa Williamson Diamond LTD, Waziri Mpango alisema kutokana na kubainika kujihusisha na udanganyifu, huku kampuni hiyo ikieleza kupata hasara kila mwaka, kuanzia mwaka huu itawajibika kutoa gawio serikalini na alimuagiza Profesa Mruma kuijulisha Bodi ya Kampuni hiyo agizo hilo la serikali mara moja.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, Lazaro Mambosasa akizungumzia agizo hilo, alisema kuwa hakuna mtuhumiwa ambaye hatoshughulikiwa katika kosa hilo.

Alisema sheria itafuata mkondo na kuwa kila mtu ambaye ameshiriki kwa namna moja au nyingine, atakamatwa kuanzia wale waliopo mgodini hadi wale walioshiriki katika kutaka kutorosha madini hayo.