SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 9 Septemba 2017

T media news

Dunia yapaza Sauti Alichofanyiwa Tundu Lissu

Matamko kutoka sehemu mbalimbali yametolewa kumuombea afya njema mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na kulaani shambulio la risasi dhidi yake na kutaka hatua kali zichukuliwe kwa waliohusika.

Lissu alipigwa risasi juzi akiwa katika gari lake mjini Dodoma na watu wasiojulikana, tukio ambalo limezua mshtuko mkubwa nchini

Spika wa Bunge, Job Ndugai jana alisema kuwa risasi zilizompata Lissu katika mwili wake ni tano; mbili mguuni, mbili tumboni na moja mkononi. Risasi 28 mpaka 32 zilishambulia gari lake.

Matamko hayo yalianza kumiminika juzi jioni wakati Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) kilipolaani kupigwa risasi kwa Lissu ambaye ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Rais wa LSK, Isaac Okero alisema tukio hilo limewashtua wanasheria wote wa Kenya.

Naye mwenyekiti wa zamani wa LSK, Eric Mutua ameiomba Serikali ya Kenya kumpa Lissu ulinzi wakati akiwa hospitalini hapo.

“Hatuna uhakika kama watu waliotaka kumuua (Lissu) nchini Tanzania, hawatafikiria kuja hapa kutimiza lengo lao. Ni muhimu kwa Serikali (ya Kenya) kuweka askari watakaomlinda kuhakikisha anakuwa salama,” alisema Mutua.

Marekani yasema ni upuuzi

Taarifa ya ubalozi wa Marekani nchini ilielezea kusikitishwa na tukio la kushambuliwa risasi mbunge huyo ikisema, “Tunalaani kitendo hiki cha kipuuzi na cha kutumia nguvu.”

Ubalozi huo ulisema unaungana na Watanzania kumtakia nafuu ya haraka Lissu ili arejee katika majukumu yake.

Ulaya, THBUB walaani

Ukiacha Wamarekani, Umoja wa Ulaya (EU) ulitoa tamko kulaaani shambulizi hilo na kutaka wahusika wake wasakwe, wakamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, EU ilisema inaungana na Serikali ya Tanzania, Bunge na vyama vya kiraia kulaani tukio hilo

“Ujumbe wa Umoja wa Ulaya unaungana na Serikali ya Tanzania, Bunge na taasisi za kiraia kulaani vikali jaribio dhidi ya maisha ya Tundu Antiphas Mughway Lissu,mbunge wa Singida Mashariki wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inasema taarifa ya EU.

Taarifa hiyo fupi inataka mamlaka ziwafikishe haraka wahusika mbele ya sheria “wale waliohusika katika shambulio hilo lisilokubalika dhidi ya demokrasia”.

Mbali na taasisi hizo, magazeti na vyombo vingine vya habari vya kielektroniki na mitandao duniani, viliripoti habari za shambulio hilo, baadhi vikihusisha na siasa na vingine vikihusisha na kesi zake alizofunguliwa hivi karibuni.

Kwa upande wake, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema tukio hilo ambalo limetokea siku chache baada ya ofisi za wanasheria wa kampuni ya Immma jijini Dar es Salaam kushambuliwa, limejenga hofu siyo kwa familia ya Lissu pekee, bali kwa wananchi wengi.

“Isitoshe, matukio haya hayaleti picha nzuri kwa nchi inayoheshimu demokrasia, haki za binadamu na utawala bora. Hivyo, tume inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha haraka upelelezi wa tukio hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria,” inasema sehemu ya taarifa ya tume hiyo iliyosainiwa na mwenyekiti wake, Bahame Nyanduga.

Amnesty International

Mbali ya kulaani tukio hilo, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeungana na wengine kuzitaka mamlaka zinazohusika kuithibitishia dunia kuwa shambulio hilo halikuwa na sura ya kisiasa.

Naibu mkurugenzi wa Amnesty wa kanda ya Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, Sarah Jackson alisema kushambuliwa kwa Lissu si tu kunatuma ujumbe wa kutaka kuwatisha watetezi wa haki za binadamu, bali pia kunaacha maswali mengi.

“Hili shambulio la kikatili dhidi ya mwanasiasa ambaye aliyeweka nyuma woga, linatia wasiwasi wa hatima ya watu wanaojitoa kwa ajili ya kutetea haki za binadamu. Mamlaka zinazohusika zinapaswa kuwajibika kwa kuueleza ulimwengu kuwa mashambulizi haya hayakufanywa kwa misingi ya kisiasa,” alisema.

Ndugai aeleza Lissu alivyojeruhiwa

Kuhusu shambulio hilo, Spika Ndugai alisema Lissu alishambuliwa kwa risasi kati ya 28 na 32, huku tano zikimpata mwilini.

Akitoa taarifa ya tukio hilo bungeni mjini Dodoma jana, Ndugai alisema risasi mbili zilimpata kwenye miguu, mbili tumboni na moja mkononi.

Alisema watu wasiofahamika wakiwa kwenye gari aina ya Nissan, walimpiga risasi kisha kutoweka.

“Baada ya tukio hilo watu hao walikimbia,” alisema.

Ndugai alisema Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa kuwa wanaishi jirani.

Alisema ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) uliandaa ndege saa 10:30 jioni kwa ajili ya kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi. Hata hivyo, baada ya kushauriana na familia na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe waliona ni vyema mgonjwa huo apelekwe  Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi.

“Hivyo kwa kushirikiana na ofisi ya Bunge ilipatikana ndege nyingine ya flying doctors (madaktari wanaofanya kazi popote) na kuondoka na mgonjwa saa 6:00 usiku kuelekea Nairobi,” alisema.

Spika alisema kuwa tukio hilo liliripotiwa polisi ambao waliahidi kufanya msako kuwatafuta watu hao na kwamba Serikali itatoa taarifa kamili kwa kuzingatia utaratibu wa kibunge.

Aliongeza kuwa tukio hilo ni la kwanza la aina yake tangu Bunge lilipohamia Dodoma na kwamba haijawahi kutokea mbunge akashambuliwa kwa risasi.

Alisema ingekuwa mbunge huyo anatakiwa kusafirishwa nje ya nchi, Serikali ina mkataba na Hospitali ya Apollo ya India na kuwa, Lissu alipelekwa Nairobi kwa sababu familia iliomba.

“Kwa nini mwenzetu alipelekwa Nairobi, ni kwa sababu familia iliomba. Nimnukuu mheshimiwa Mbowe kwa niaba yake si kwamba wana shaka na umahiri na uwezo wa madaktari wetu,” alisema  Ndugai.

Pia, aliwataka Watanzania kuendelea kumuombea kiongozi huyo katika kipindi hiki kigumu na kuwawashauri wabunge walioanza kutuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kutumia maneno ya hekima badala ya kuendelea kuzichonganisha pande mbili.

Wabunge wajawa hofu

Wakizungumzia tukio hilo, wabunge wamevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kuhakikisha kuwa matukio ya aina hiyo yanadhibitiwa.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Ritta Kabati alisema malalamiko yamekuwa mengi na ndio maana Bunge limeona kuna umuhimu wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kukaa na vyombo vya usalama kujua sababu za matukio yasiyoeleweka.

“Mtu kavamiwa unasikia kuwa wanafanya upelelezi halafu baadaye hatupati mwisho wake ni nini? Tukio la Lissu linasikitisha sana. Tukio hili limetuchanganya akili, kumbe hatuko salama sana,” alisema.

“Limetokea katika jengo la mawaziri, naibu spika na wabunge. Huwa tunaamini kuna maaskari (maeneo hayo), lakini nao wamepitwa.”

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma alisema tukio hilo limemsikitisha hasa ikizingatia kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi na kwa hiyo Serikali yote iko hapo na Bunge linaendelea na vikao vyake, lakini mbunge akapigwa risasi na watu hawajulikani.

“Kimsingi ni jambo ambalo linatia simanzi sana hasa upande wetu  kama wabunge kwa sababu leo ni kwa Tundu Lissu, kesho mimi keshokutwa kwa mwingine hatuwezi kujua,” alisema.

Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete alisema mshtuko mkubwa alioupata ni kwa sababu katika jamii alitegemea mbunge angekuwa mtu salama zaidi, lakini anashambuliwa na kuhoji kuwa usalama wa wananchi mitaani ukoje.

“Lakini pili niuombe sana umma katika kipindi hiki kizito wawe watulivu kwa sababu haya mambo yanapotokea yanaweza kuwa na sura nyingi na tafsiri nyingi,” alisema.

“Lakini tuviamini vyombo vyetu vitatuletea majibu sahihi ambayo yatatoa  mwanga jinsi gani limetokea, ukweli na kuona tunatokaje kuanza hapa.”

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alisema Lissu ni miongoni mwa wabunge waliolalamika kufuatiliwa na magari na hadi akataja namba, rangi na idadi ya watu waliokuwa wakimfuatilia, lakini kinachomsikitisha hakuona kama jambo hilo lilipuuzwa.

“Sasa Bunge limepeleka katika kamati, ninaamini baada ya pale hatua zitachukuliwa,” alisema.

“Tusipokomesha, jambo hili linajenga chuki kati ya Watanzania na Serikali yao, kati ya Watanzania na chama kilichounda Serikali, lakini linapeleka sura mbaya duniani.”

Mbowe awatoa hofu wananchi

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Lissu ni mzima, lakini hayuko katika hali nzuri.

Mbowe alisema hafikirii kama wahuni ndiyo waliofanya shambulio hilo kwa kuwa Lissu hana maadui nje ya siasa.

“Tunashuku kuna msukumo wa kisiasa katika shambulio hili, ikizingatiwa silaha nzito iliyotumika na idadi ya risasi zilizofyatuliwa. Ni wazi wahusika walikuwa na nia ya kumuua na sio kumuibia au kuchukua chochote kutoka kwake,” alisema.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisema katu wanachama wa chama chake hawataogopa kupaza sauti na wataendelea kupambana kuhakikisha demokrasia inasimama.

Vyombo vya habari kimataifa

Baadhi ya magazeti yaliyoripoti tukio hilo la Lissu ni Independent Times la Uganda, Daily Nation la Kenya, Newyork Times la Marekani na mashirika mbalimbali ya habari.

Imeandikwa na George Njogopa, Elizabeth Edward, Tumaini Msowoya, Sharon Sauwa na Aggrey Omboki