SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 15 Agosti 2017

T media news

Vijue viwanda viwili vikubwa vitakavyojengwa na Misri nchini Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi leo tarehe 15 Agosti, 2017 amemaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku 2 aliyoifanya hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais El-Sisi ameagwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Mhe. Rais El-Sisi ameondoka nchini na kuelekea nchini Rwanda ambako anaendelea na ziara yake.

Akiwa hapa nchini, hapo jana Mhe. Rais El-Sisi amefanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam na baadaye viongozi hao wakazungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.

Pamoja na kuzungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili viongozi hao wamekubaliana kuwa kamati ya pamoja ya nchi hizi (Joint Permanent Commission – JPC) iliyokutana mara ya mwisho miaka 20 iliyopita, ikutane haraka iwezekanavyo ili kuongeza msukumo katika masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano hususani katika uchumi na biashara.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais El-Sisi kwa kukubali kujenga kiwanda kikubwa cha nyama hapa nchini, ili kuwawezesha wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao, na pia kukubali kujenga kiwanda cha dawa za binadamu kwa kuwa Tanzania inaagiza dawa nje ya nchi kwa asilimia 100.

“Nimemuomba Mhe. Rais El-Sisi na amekubali kuwa watajenga viwanda hivi, naamini viwanda hivi vikijengwa hapa nchini kwetu nchi zetu mbili zitapata faida, sisi tutapata ajira nyingi, Serikali itaokoa fedha nyingi inazotumia kuagiza dawa nje, wafugaji wetu ambao wanashika nafasi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika watapata soko, Serikali itakusanya kodi lakini na wenzetu Wamisri watapata nyama na faida ya uwekezaji wao hapa nchini kwetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu biashara Mhe. Rais Magufuli amesema kwa sasa thamani ya biashara ya Tanzania na Misri ni kiasi kidogo cha Dola za Marekani Milioni 78.098, uwekezaji wa Misri hapa nchini umefikia Dola za Marekani Milioni 887.02 na umezalisha ajira 953, hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini humo kuja hapa nchini kuwekeza na kwamba Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha.

Mhe. Rais Magufuli pia amemshukuru Mhe. Rais El-Sisi kwa kukubali kushirikiana na Tanzania kukuza utalii na usafiri wa anga na amesema Tanzania ambayo inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na vivutio vingi duniani inaweza kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio hivyo ikilinganishwa na hali ya sasa ambapo ni watalii Milioni 2 tu wanakuja Tanzania kwa mwaka.

Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Mhe. Rais El-Sisi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi zote zinazohusika na mto Nile kutekeleza makubaliano ya matumizi bora ya mto huo yanayozingatia maslahi ya nchi zote huku ikitambua kuwa mto huo ndio moyo wa Misri.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais El-Sisi kwa mchango mkubwa ambao nchi hiyo inautoa kwa Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, miundombinu, elimu, kilimo na utawala bora.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

15 Agosti, 2017