SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 31 Agosti 2017

T media news

Picha: Amiri Jeshi Mkuu, Rais Magufuli akutana na Wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 31 Agosti, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wastaafu na viongozi wa sasa wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini.

Viongozi hao ni Wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Wakuu wa Jeshi la Polisi, Wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Wakuu wa Idara ya Uhamiaji, Wakuu wa Jeshi la Magereza na Wakuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Baada ya mazungumzo hayo viongozi wastaafu wa vyombo vya ulinzi na usalama wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwaita na kufanya nao mazungumzo, ambayo yamewawezesha kubadilishana mawazo na kuimarisha zaidi ushirikiano kati yao na viongozi wa sasa wa vyombo hivyo.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Magufuli na tunampongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya, sio jambo la kuficha amefanya kazi nzuri, na kila mmoja wetu amezungumza hilo na tunamtakia kila la heri ili aweze kuendeleza pale alipofika, kwa kweli tumefurahi sana” amesema Bw. Cornel Apson, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Mstaafu.

“Tumeona ni jambo jipya na halijawahi kutokea kwa Rais kutuita viongozi wastaafu, nchi yetu chini ya Mhe. Magufuli inakwenda vizuri, Watanzania tuiunge mkono Serikali hii kwa sababu inatuelekeza mahali kuzuri”amesema Jenerali Mstaafu Robert Mboma, Mkuu wa JWTZ Mstaafu.

Viongozi hao wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uendeshaji mzuri wa Serikali, hususani katika kusimamia uchumi, kupiga vita rushwa, kujenga nidhamu kwa watumishi wa umma na wamemuahidi kuendeleza zaidi ushirikiano na viongozi waliopo sasa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa amesema Mhe. Rais Magufuli amekutana na viongozi hao kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano imara zaidi kwa viongozi wastaafu na viongozi wa sasa katika kutekeleza majukumu ya ulinzi na usalama wa nchi.

“Mhe. Rais Magufuli amefurahishwa sana na mwitikio wa viongozi hawa wastaafu wa vyombo vya ulinzi na usalama na amewahakikishia kuwa Serikali anayoiongoza itaendeleza ushirikiano nao ili kunufaika na uzoefu wao” amesema Bw. Msigwa



Jaffar Haniu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

31 Agosti, 2017