SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 16 Agosti 2017

T media news

Mama yangu aliuza pombe ili apate ada yangu ya shule’ – Simbu

Kuna usemi usemao ‘mafanikio hayaji kirahisi, lazima uyapambanie’. Usemi huu unakamilishwa na mtanzania aliyeshinda medali ya shaba kwenye mashindano ya IAAF World Championship 2017 Alphonce Felix Simbu ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu.

Simbu licha ya kuzaliwa na kulelewa katika familia yenye maisha magumu hakuacha kupambana kwa kile anachokiamini na hatimaye amefanikiwa kupata medali kwenye mashindano ya riadha ya dunia.

Mkimbiaji huyu amesimulia kwa ufupi maisha aliyopitia katika familia yake licha ya vikwazo na magumu kadhaa lakini hakukata tamaa kwa kile alichokiamini.

“Wakati nasoma nilipokuwa nikirudi nyumbani kwa ajili ya likizo, nilikuwa nachelewa kurudi shule kwa sababu ya kukosa ada. Mama alikuwa anauza pombe ili apate pesa ya kulipa ada.”

“Baba alikuwa akisaidiana na mama kuchota maji kwa ajili ya kuandaa pombe, walikuwa wanasaidiana kuhangaika kwa ajili yangu.”

“Huwezi amini, nilikuwa naiombea pombe ili iwe nzuri mama auze apate pesa ili mimi niwahi shule.”

Mwaka 2016 Simbu alihojiwa na Shaffih Dauda kwenye mashindano ya Olympic Rio 2016 nchini Brazil akasema, lengo lake ni kuwa bingwa wa Dunia wakati huo alimaliza katika nafasi ya tano.

Watanzania wote wanafurahia medali ya Simbu, hakika amelipambania taifa na kurudi na heshima kubwa. Hongera Alphonce Simbu.