Mgombea anayepeperusha bendera ya Muungano wa NASA (National Super Alliance) katika uchaguzi mkuu wa Kenya, Raila Odinga amesema kuwa Rais Dkt Magufuli wa Tanzania atamsikiliza yeye zaidi kuliko atakavyomsikiliza Rais Uhuru Kenyatta.
Akizungumza na wananchi wa Mji wa Namanga katika eneo la Kajiado Ijumaa Julai 28, alisema kuwa yeye ni rafiki wa karibu wa Rais Magufuli na hivyo atatumia urafiki huo kuhakikisha kuwa anaimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Kenya ambao kwa sasa umeyumba kidogo kuhusu masuala ya kibiashara.
Alisema pia, mara tu atakapochaguliwa kuwa Rais, Tanzania itaiondolea Kenya vikwazo ilivyoiwekea katika usafirishaji wa bidhaa.
“Magufuli ni rafiki yangu, nitazungumza nae kuhakikisha kuwa mpaka huu (Namanga) unafunguliwa,” alinikuliwa Raila ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya katika kipindi cha serikali ya mpito.
Raila Odinga na Magufuli wamekuwa marafiki kwa muda mrefu sasa kitendo kilichopelekea kuwapo kwa madai kuwa Tanzania imeiruhusu NASA kuweka kituo cha kujumlishia matokeo nchini. Lakini tuhuma hizo zilikanushwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ambapo ilisema Tanzania inaheshimu na haitoingilia uchaguzi huo.
Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu ambapo mchuano mkali upo kati ya Rais wa sasa, Uhuru Kenyataa anayepeperusha bendera ya Muungano wa Jubilee na Raila Odinga wa NASA.