Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa la Tanzania Ndg. Paul Sozigwa aliyefariki dunia leo tarehe 12 Mei, 2017 Jijini Dar es Salaam.
Katika Salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Marehemu Paul Sozigwa atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka kwa Taifa, uchapakazi na uadilifu.
“Natambua kuwa Marehemu Paul Sozigwa ni miongoni mwa Waasisi wa Taifa letu ambao walijitoa kwa dhati kuipigania nchi yetu kabla na baada ya uhuru, alishirikiana na Waasisi wengine wa Taifa letu akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizolikabili Taifa letu baada ya uhuru zikiwemo kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi ndani yaChama na Serikali, hakika tutazienzi juhudi zake” amesema Mhe. Rais Magufuli.