SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 30 Aprili 2017

T media news

MBUNGE CCM Atuhumiwa Kuhujumu Uchumi..Akwepa Kulipa Kodi ya Milioni 500..!!!


MBUNGE wa Kwimba, Mwanza, Shannif Mansour (CCM), anatuhumiwa kugoma kulipa kodi ya eneo lake la ardhi lenye ukubwa wa hekta 39,000, kiasi cha zaidi ya Sh. 500 milioni tangu mwaka 2010.

Mansour kupitia kampuni yake ya Sineji Tanzania Limited, anatuhumiwa kuigomea serikali kulipa kiasi hicho cha fedha kwa madai yeye hawezi kulipa fedha hizo kwa kuwa anafahamiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi.

Eneo hilo la Mansour na kampuni yake inayojihusisha na utengenezaji wa malighafi za ujenzi ikiwemo kusaga kokoto, lililopo kata ya Buhongwa, Nyamagana pia baadhi ya wananchi wanalalamika kulaghaiwa fedha za fidia za maeneo yao.

Tangu kipindi hicho, mbunge huyo alikuwa anadaiwa kiasi cha Sh. 529 milioni na Halmashauri ya jiji la Mwanza na kwamba wakati alipotakiwa kulipa fedha hizo tangu mwaka 2010 alikuwa akigoma kulipa fedha hizo kwa kutumia mwamvuli wa nafasi yake ya ubunge.

Madai ya mbunge huo kuigomea serikali kulipa kodi hiyo, yaliibuliwa jana na Waziri Lukuvi, wakati alipokuwa akizungumza na wakuu kitengo cha idara ya ardhi na wakuu wa vitengo vingine katika Jiji la Mwanza.

Akizungumza katika kikao hicho, Lukuvi amesema kuwa anashangaa kusikia mbunge huyo akigoma kulipa fedha hizo huku watendaji wa halmashauri hiyo wakishindwa kuchukua hatua za haraka ili kada huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alipe kodi ya serikali.

Amesema kuwa katika ulipaji wa kodi wa ardhi watumishi wa idara hiyo wanapaswa kuacha kuangalia kabila wala chama cha mtu kwani waziri hana mamlaka ya kufuta utaratibu wa ulipaji wa kodi lazima ufuatwe.

Hata hivyo, amesema kuwa watumishi hao wanapaswa kuhakikisha ifika Mei 2, mwaka huu wawe wamemchukulia hatua ikiwemo kuangalia utaratibu wa kufuta hatimiliki ya mbunge huyo ili waweze kumuuzia mtu mwingine na kupata mapato.

“Nusu ya lengo lenu la ukusanyaji wa mapato unachangiwa na mtu mmoja (Mansour), haiwezekani mtu mmoja akatae kulipa kiasi hicho cha fedha na nyie mnachelewa kuchukua hatua, utaratibu wa sasa hakuna atakayeshindwa kuchukuliwa hatua kama atashindwa kulipa kodi.

“Eneo lenye ukubwa wa hekta 39,000 sawa na hekari 96, mtu anakataa kulipa kodi, naagiza ikifika, Mei 2, mwaka majibu ya suala hili yawe yamepatikana mara moja, mbunge gani ambaye hataki kulipa kodi,” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema kuwa watendaji wa ardhi jijini hapa, wamekuwa wakishindwa kuwadai kodi wafanyabiashara wakubwa na badala yake wamekuwa wakikusanya kutoka kwa watu wa chini na kuagiza tabia hiyo kukoma.

Afisa Ardhi Mteule Jiji la Mwanza, Silvery Salvatory, amesema kuwa tayari wameisha mchukulia hatua ikiwemo kumfikisha katika baraza la usuruhishi la ardhi mkoani hapa na uamzi wake unatarajiwa kutolewa Mei 5, mwaka huu.