Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMKF), Rais Mstafu Dkt Kikwete leo atazindua taasisi yake hiyo mpya jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya JMKF ilieleza kuwa taasisi hiyo itakuwa imejikita katika kusaidia nyanja kuu ikiwa ni Maendeleo, Afya, Amani, Elimu na Utawala Bora.
Baada ya chakula cha mchana leo, Rais Mstaafu Dkt Kikwete atazungumza na vyombo vya habari ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu alipotoka madarakani Novemba 5, 2015. Aidha, Rais Kikwete atafanya uzunduzi huo na kuongoza kikao cha Bodi ya Wadhimini kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Rais Kikwete ameamua kujikita katika masuala ya maendeleo endelevu, afya, elimu na utawala bora ikiwa ni nyanja ambazo alizishughulikia zaidi katika kipindi cha miaka 10 alipokuwa Ikulu. Hata kabla ya kuwa Rais, Dkt Kikwete alijikita katika kuboresha maisha ya watu kila mara alipopata nafasi ya kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya watu, ndio sababu bado ana matumaiani kuwa JMKF itaboresha maisha ya watu.
JMKF imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi na itafanyakazi chini ya Bodi ya Wadhamini ya Kimataifa ambayo inaundwa na wajumbe kutoka ndani na nje ya nchi ambapo ni pamoja na Marekani, Malaysia na Guinea Bissau.
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ni Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Ombeni Sefue, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza Mukandala, Daktari Bingwa wa Upasuaji Profesa William Mahalu na aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Marekani, Balozi Mwanaidi Maajar.
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Carlyle ya Afrika Kusini, Genevive Sangundi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Abubakar Bakhresa.
Wajumbe wa Bodi kutoka nje ya Tanzania ni Balozi Charles Stith kutoka Marekani ambaye alikuwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dato Sri Idris Jala kutoka Malaysia ambaye ni Waziri asiye na wizara maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia na Mkurugenzi Mtendaji wa Matokeo Makubwa Sasa nchini humo.
Mjumbe mwingine kutoka nje ya nchi ni Dr Carlos Lopez kutoka Guinea Bissau ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).