Watu waliofariki dunia, waliohama na wasiofahamika wilayani Rorya mkoani Mara, wamemchanganya mkuu wa wilaya hiyo Simon Chacha kuendelea kunufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini.
Mpango huo ambao unaendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), umebaini wati 112 wasiotakiwa kunufaika nao, lakini walikuwa wakivuna fedha za ruzuku kila zitolewapo.
Chacha amesema kuanzia sasa hataki kusikia kwamba kuna watu wa aina hiyo ambao wanatumia jasho lisilowahusu kunufaika nalo na kwamba, hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea kaya maskini katika Kijiji cha Nyabikondo kilichopo Kata ya Kinyeche na Kijiji cha Ryaghati katika Kata ya Nyahongo wakati wa utoaji na upokeaji fedha kwa kipindi cha Machi na April 2017, mwaka huu.
Akiwa Kijiji cha Nyabikondo, Chacha alihoji baadhi ya wananchi wanaonufaika na fedha ambapo alibaini baadhi ya majina ya walengwa waliofariki akiwamo Victoria Obimbo ambaye alikuwa akipokea ruzuku ya Sh20,000 na alifariki mwezi Januari, 2017 lakini fedha zake zinaendelea kuchukuliwa na ndugu yake.
“Naombeni kama mnajua kuna watu walifariki na majina yao yanaendelea kupokewa fedha semeni, haiwezekani pesa ilikuwa inatolewa kwa mlengwa husika halafu akafariki, lakini wanamchukulia pesa mtu akishafariki na mgao wake unakuwa umekoma,” amesema Chacha
Baadhi ya wanufaika akiwamo Sophia Ochora wamelalamika kuku kufa kwa ugonjwa na mwingine Julia Majengo amedai kondoo wake wawili waliliwa na hivyo ndoto zake kutotimia.
Mratibu wa Tasaf wilayani Rorya, Ayoub Mrimi amesema kuwa wamepokea fedha za kaya maskini Sh254 milioni zitakazonufaisha vijiji 52 kati ya vijiji 87 vyenye kaya 7,241 zilizothibitshwa kuingizwa kwenye mpango huo.