Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewaomba wanachama wa CCM wanaoanza mkutano mkuu wao maalumu kesho, kuweka mbele uzalendo badala ya ushabiki wa kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema wanachama wa CCM wanapaswa kuutumia mkutano huo kuisema Serikali yao kuhusu kupuuza mambo ya msingi, ikiwamo malengo ya bajeti iliyopitishwa na Bunge.
Alisema imekuwa kawaida kwa Serikali kupuuza mambo ya msingi na kufanya ambayo hayamo kwenye bajeti huku baadhi ya maeneo yakikosa huduma muhimu.
Dk Mashinji alitoa mfano kuwa, mwaka wa bajeti wa 2016/17 unakaribia kwisha, lakini kiuhalisia utekelezaji wake uko robo ya nne na haujafikia asilimia 40.
Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema mbali na hayo, Serikali haitaki kusimamiwa kikamilifu na inauyumbisha mhimili wa Bunge ambapo vikao vya kamati za Bunge vimeshindwa kuanza kama ilivyopangwa awali kwa wiki tatu, badala yake muda umepunguzwa hadi wiki mbili. Aliongeza kwamba bajeti iliyopitishwa imekuwa haiheshimiwi na kuingiziwa matumizi ambayo hayakuwemo ikiwamo Serikali kuhamia Dodoma, kujenga kiwanja cha ndege Chato na Magereza ya Ukonga