Baada ya taarifa ya Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge chini ya mtani na kaka yangu Kepteni Mstaafu George Huruma Mkuchika kukabidhiwa kwa Spika, Spika ataiweka taarifa hiyo katika ratiba za shughuli za Bunge ili iwasilishwe na kujadiliwa. Tayari Mkuchika na Kamati yake wameshakamilisha taarifa yao tayari kuikabidhi kwa Spika, Ndugu Job Justino Ndugai.
Taarifa hiyo inatarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa kati ya leo au kesho. Taarifa ya Kamati ya Mkuchika itabeba kilichopatika katika mahojiano na Makonda; maoni na mapendekezo ya Kamati. Makonda (Daudi Albert Bashite) aliitwa kuhojiwa na Bunge kupitia Kamati hiyo kwa kulidharau Bunge kupitia kauli zake za kejeli na kiburi alizozitoa juu ya Bunge na Wabunge.
Katika hali ya 'kudhibiti' kauli na mwenendo wa Wabunge wa CCM kuhusu taarifa hiyo, viongozi wa Wabunge wa CCM wameanza kuwapanga Wabunge wa CCM. Kuwapanga huko kunaratibiwa na Katibu wa Wabunge wa CCM, Ndugu Jason Rweikiza. Rweikiza, kwa mujibu wa taarifa toka Dodoma, anawataka Wabunge kupongeza hatua ya Makonda ya kuomba msamaha kwa barua.
Imeelekezwa kuwa kama Rweikiza na timu yake watakwama kuwapanga Wabunge wa CCM kuhusu taarifa hiyo, basi kutalazimu kuwepo kwa Kikao cha Wabunge wote wa CCM almaarufu kama Party Caucus ili Wabunge waandaliwe na utaratibu wa kuwamulika mjadala utakapoanza uwekwe. Maandalizi ya haraka ya Caucus yatafanyika.