Rapper Nay wa Mitego, Alhamis hii aliitikia wito wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe kukutana naye mjini Dodoma kwaajili ya kuzungumza namna ya kuuboresha wimbo wake Wapo ambao licha ya kuikosoa vikali serikali pamoja na Rais Dkt John Magufuli umepokelewa kwa mikono miwili.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Rais Magufuli kuamuru kuachiwa huru kwa Nay ambaye alikuwa amekamatwa na polisi na wimbo wake kufungiwa na BASATA. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Dkt Mwakyembe alisema wasanii wana nafasi kubwa katika kuisaidia serikali kukemea mambo maovu.
Amewataka vijana kutambua kuwa Tanzania ni nchi inayozingatia utawala wa sheria na kwamba wana uhuru wa kukosoa bila kutukana au kwenda nje ya maadili. “Na ndio maana tukasema kwa wimbo wa Nay hapana, hebu ngoja tuusikie, mbona ni wimbo mzuri tu,” alisema Mwakyembe.