Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema matukio yaliyotokea hivi karibuni likiwamo la aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kutolewa bastola, yanaweza kubadili upepo wa Bunge linalotarajiwa kuketi siku chache zijazo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, aliwaambia hayo waandishi wa habari jana waliotaka kufahamu mipango ya chama hicho katika kutumia mhimili wa Bunge kutokana na uwepo wa matukio ya uvunjaji wa sheria.
Katika hilo, Mnyika alisema Watanzania watarajie Bunge lijalo la Bajeti kuwaka moto.
“Sisi ndio tunaongoza Kambi Rasmi ya Upinzani na ambacho ninaweza kuwaambia Watanzania ni kwamba watarajie Bunge la Bajeti kuwaka moto juu ya utendaji wa Serikali. Sasa kuwaka moto namna gani na kuhusu nani ni masuala ambayo yataonekana katika hatua ya baadaye. Naamini safari hii haitakuwa wabunge wa Chadema, Ukawa pekee, naamini Bunge litakuwa kitu kimoja katika kuchukua hatua,” alisema Mnyika.
Chadema Yanunua Ugomvi wa Nape
Katika hatua nyingine chama hicho kimemtaka Rais Dk. John Magufuli ajitokeze waziwazi na kusema sababu za kumwondoa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Pamoja na hilo, kimetaka Rais Dk. Magufuli aseme iwapo alitoa maelekezo kwa vyombo vya usalama waliovamia ofisi za Clouds Media Group na yule aliyemtolea bastola Nape alipokuwa akizuia asizungumze na vyombo vya habari juzi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, aliyezungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuhusu ajenda mbili zilizozungumzwa katika kikao cha Kamati Kuu Maalumu ya chama hicho kilichoketi Machi 22 na 23, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
“Ni vyema Rais akaeleza kwa kuwa taarifa za Ikulu hazikufafanua kwanini amemwondoa Nape. Aeleze waziwazi sababu za kumwondoa Waziri katika kipindi ambacho taarifa ya kamati iliyoundwa imetolewa ambayo imeeleza wazi makosa yaliyofanywa na mteule wa rais katika siku chache tu baada ya kumkingia kifua.
“Imeonekana matumizi mabaya ya wazi ya watumishi wa vyombo vya usalama ikiwamo waliovamia kituo cha Clouds kwa bunduki, aliyemtolea Nape bastola, rais ndiye msimamizi wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama, awaeleze Watanzania iwapo askari na wanausalama hao wamefanya kazi kwa maelekezo yake,” alisema Mnyika.
Alisema kama sivyo ni hatua zipi ameelekeza zichukuliwe kwa wahusika wa mambo hayo.
Mnyika alisema chama hicho kinapinga mwenendo wa matumizi mabaya ya madaraka ikiwa ni pamoja na kulindwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na matukio ya hivi karibuni yanayogusa uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group pamoja na kitendo cha Nape kutolewa bastola.
“Uamuzi wa kumlinda Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa gharama hata ya kumwondoa Waziri wake ni wazi ni matumizi mabaya ya madaraka. Na matumizi haya mabaya ya madaraka yamejipenyeza sasa hayamhusu Rais tu pekee bali pia watendaji wake na vyombo mbalimbali,” alisema Mnyika.
Alisema nchi imeanza kuwa ya kipolisi na matumizi ya vyombo vya dola katika masuala ambayo havipaswi kutumika.
“Tunatoa pole kwa wanahabari kwa mambo hayo pamoja na Nape kwa haya yanayomkuta,” alisema Mnyika.
Alisema haki inapovunjwa mahali popote na kwa raia yeyote, wao kama chama hawasiti kutoa kauli ya kukemea.
Mnyika aliwataka Watanzania kuungana kupinga mabaya yanayofanywa na Serikali ili kulinusuru Taifa na hatari zinazoikumba na zitakazoendelea.
“Taarifa nilizonazo kutoka vyanzo vyangu serikalini ni kwamba, Rais ameamua kumlinda RC kwa sababu eti Chadema kupitia kwa Mwenyekiti Mbowe ilitoa msimamo wa kumtaka amchukulie hatua. Watu ndani ya Serikali wanasema kama atamchukulia hatua eti Rais ataonekana amekidhi matakwa ya Chadema,” alisema Mnyika.
Alisema chama chao kina wajibu wa kuikosoa Serikali iwapo haifanyi kazi sawa sawa na Rais anawajibika kwa wananchi na si Chadema.
Mnyika alikumbusha kuwa wakati walipotangaza Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), waligusia kauli kuwa; anapoonewa yeyote, unapokuwa kimya, haki inapovunjwa kwa mtu mmoja ukadhani kwamba haikuhusu, ikaenda kuvunjwa kwa mtu mwingine ukanyamaza kimya ukadhani kwamba haikuhusu, ipo siku jambo litakukuta mwenyewe na hakutakuwa na mtu wa kupaza sauti kwa niaba yako.
Alisema kauli hii ilionekana kuwahusu upinzani pekee lakini hivi sasa imejidhihirisha tofauti kutokana na athari zinazojitokeza kwa raia, vyombo vya habari na baadhi ya wanaCCM.