Timu ya maafande wa JKT Ruvu hatimaye imepata ushindi wake wa kwanza tangu kuanza kwa mwaka 2017 baada ya kuifunga Mbao FC bao 2-0 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.
Mara ya mwisho JKT Ruvu kupata ushindi ilikuwa ni October 29, 2016 ipoifunga Ndanda FC kwa bao 1-0.
Baada ya hapo, ilijikuta ikicheza mechi tisa (9) bila kupata ushindi. Ushindi ambao walikuwa wakisherekea ni sare pekee, lakini vichapo ndio vilikuwa vimetawala zaidi kwao.
02/11/2026 Majimaji 1-0 JKT Ruvu
06/11/2016 JKT Ruvu 1-1 Toto Africans
17/12/2016 JKT Ruvu 0-3 Yanga
24/12/2016 Simba 1-0 JKT Ruvu
01/01/2017 African Lyon 0-0 JKT Ruvu
13/01/2017 JKT Ruvu 1-1 Ruvu Shooting
30/01/2017 JKT Ruvu 0-0 Stand United
04/02/2017 Mbeya City 2-0 JKT Ruvu
08/02/2017 Tanzania Prisons 2-1 JKT Ruvu
12/02/2017 JKT Ruvu 2-0 Mbao FC
Katika mechi hizo tisa, walipoteza mechi tano (5) na kutoka sare katika michezo minne (4) hivyo kuambulia pointi nne kati ya 27 walizokuwa wakiziwania katika michezo hiyo tisa.
JKT Ruvu ambao wamehamishia makazi yao mkoani Tanga walifunga magoli yao dakika ya 28 kupitia Atupele Green aliyepachika bao hilo kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Mbao FC Boniface Maganga kuunawa mpira kwenye box akiwa katika harakati za kuokoa mpira kujaa wavuni.
Bao la pili la JKT Ruvu likafungwa na Hassan Dilunga dakika ya 54 akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Najim Magulu.
JKT Ruvu wamefikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi 23 huku wakiendelea kusalia mkiani (nafasi ya 16) kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara.