SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 13 Februari 2017

T media news

Chadema Watoa Tamko Rasmi Juu ya Anayoyafanya Makonda,Wamtaka Magufuli Amuonye,La Sivyo...!!!


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Ziwa Victoria kimemuomba Rais John Magufuli kumkanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ili asije kuliangamiza Taifa kwa ilichodai kutafuta sifa za kisiasa.

Pia, chama hicho kimesema Taifa kwa sasa linakumbwa na ugonjwa wa kisiasa hali inayoweza kuliangamiza kama isipokemewa na anachofanya Makonda kinapaswa kupingwa vikali na asasi zote ikizingatiwa kwamba Tanzania ni nchi ya kidemokrasia.

Akizungumza kwa na wanahabari kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ansebert Ngurumo alisema kinachofanywa na  Makonda ni kutafuta vyeo kwa sifa kwani tangu mwanzo amekuwa akipata vyeo kupitia 'propoganda' za kisiasa bila kutambua yeye ni kiongozi wa kiserikali kwa sasa.

Ngurumo ambaye aliwahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, alisema Taifa imekumbwa na ugonjwa wa ukakasi unaowapata viongozi wa kisiasa wanaoitwa Demagobi.

"Demagogi ni neno la kigiriki, Demo- watu halafu Gogi- viongozi wanaongoza watu kwa kutafuta sifa kama akina Makonda. Namuomba Rais Magufuli amkanye asije liingiza taifa sehemu mbaya kwa kutafuta sifa," alisema.

Akizungumza kwa kutoa mfano, Ngurumo alisema Joseph McCarthy ambaye alikuwa Senator katika Bunge la juu Marekani (Senate) 1947 wakati vita baridi ilipopamba moto, alibuni mbinu ya kupata umaarufu.

Alisema ana orodha ya Wamarekani wanaoisaliti nchi yao kwa kuwa Wakomunisti na pengine kufanya upelelezi (espionage) kwa niaba ya Urusi kitu ambacho kipindi kile si tu kinamaliza wengine kiheshima, lakini pia kinaweza kusababisha hata kunyang'anywa uraia.

Ngurumo alisema McCarthy alitaja majina kutoka katika vikaratasi na alipambwa na kupendwa na sehemu ya umma wa Marekani kwa kuwa kipindi hicho vita dhidi ya USSR ilibeba hisia kali, ambapo watu hukuweza kuwaambia kitu.

“Huo ndiyo 'ujasiri' aliojifanya anao Senator McCarthy, mpaka kujifaragua kumtaja Waziri Mkuu wa nchi nyingine, huku baadhi ya wananchi wa US hadi waliandamana kutaka Senator McCarthy apewe tuzo kwa 'kuongoza mapambano yaliyotukuka dhidi ya maadui wa US',” alisema.

Katika hatua nyingine, Ngurumo alivitaka vyombo vya habari kuacha kukuza jambo hilo kwani si mara ya kwanza taifa kuwa na matukio ya maajabu.

"Mwaka 2013 aliibuka babu wa Loliondo kuwa anatibu magonjwa sugu na taifa zima lilihamia kwa babu wakiwemo viongozi wakubwa kisiasa, dini na wengineo, huku jambo hilo likiwa imekuzwa na ‘media’ hivyo nawaomba wanahabari wenzangu fanyeni utafiti kwanza," alisema.