SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 27 Januari 2017

T media news

Watu 14 akiwamo Mchina wafukiwa mgodini Geita

Watu 14 akiwemo Mchina, wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa katika mgodi wa dhahabu wa Kampuni ya RZ Union Mining Ltd uliopo Kata ya Nyarugusu mkoani Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga jana alisema watu hao wamefukiwa chini ya mgodi baada ya mlango wa kuingilia kwenye shimo la mgodi kumeguka udongo na kujiziba.

“Usiku wa kuamkia leo (jana) saa tisa kwenye mgodi huo unaoendeshwa na Wachina, mlango wa kuingilia mgodini mmoja ulimeguka na kujifunga watu 14 wakiwa ndani,” alisema Kyunga.

Kyunga alisema kwa mujibu wa kitabu cha orodha ya watu wanaojiandikisha kuingia mgodini, kuna majina ya Watanzania 12 na Mchina.

Aidha, alisema mbali na watu hao 13, pia kuna Mtanzania mmoja ambaye aliingia bila kujiandikisha na hiyo ni kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo hivyo kufanya idadi ya watu waliofukiwa kuwa 14. 

Kyunga alisema tangu jana asubuhi jitihada mbalimbali za kuondoa udongo kuwaokoa watu hao zinaendelea wakitumia mitambo na wataalamu.

“Kwa kusaidiana na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) na wataalamu wengine, jitihada zinaendelea ili kuhakikisha tunawaokoa watu hao,” alisema Kyunga. 

Alisema wakati huo huo wamefanikiwa kutoboa eneo jingine na kupitisha mabomba ya hewa ya oksijeni ili kuwafanya watu hao wasikose hewa.