Na Baraka Mbolembole
KATIKA misimu 6 iliyopita ya Ligi kuu Tanzania Bara, Azam FC imetoa washindi watatu katika tuzo ya mfungaji bora VPL. Mrisho Ngassa alikuwa mchezaji wa kwanza wa Azam FC kushinda tuzo hiyo msimu wa 2010/11.
Ngassa alifunga jumla ya magoli 16. Nahodha wa Azam, John Bocco akairudisha tuzo hiyo Azam Complex Chamanzi msimu wa 2011/12 baada ya kufunga magoli 16, kisha Muivory Coast, Kipre Tchetche akatengeneza historia ya tuzo hiyo kuchululiwa mara tatu mfululizo na wachezaji wa timu hiyo iliyoanzishwa miaka 9 iliyopita. Kipre alifunga magoli 14 na kushinda tuzo hiyo msimu wa 2012/13.
Baada ya hapo hakuna mchezaji yeyote wa Azam FC aliyetoa changamoto katika tuzo hiyo. Msimu wa 2013/14 ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza VPL, Mrundi, Amis Tambwe akafanikiwa kushinda tuzo hiyo baada ya kufunga magoli 19 akiwa na kikosi cha Simba SC.
Tambwe ambaye sasa ni mchezaji wa Yanga anaungana na Abubakary Mkangwa na Abdallah Juma kushinda tuzo hiyo zaidi ya mara moja tangu mwaka 2000. Saimon Msuva alifunga magoli 17 na kushinda tuzo ufungaji bora msimu wa 2014/15. Tambwe akarejea tena na kushinda tuzo hiyo msimu uliopita baada ya kufunga magoli 21.
Kwa misimu miwili mfululizo mfungaji bora wa VPL amekuwa akitoka katika kikosi cha Yanga. Je, watafikia rekodi ya Azam FC kutoa wafungaji bora mara tatu mfululizo?
Katika orodha ya wafungaji msimu huu, Msuva anashikilia nafasi ya kwanza akiwa amefunga magoli 9 sawa na kiungo mshambulizi wa Simba, Shiza Kichuya na kwa karibu wanafuatwa na wafungaji, Tambwe anafuata kwa m,agoli 8 na Rashid Mandawa anayechezea Mtibwa Sugar ana magoli 7.
Kulingana na mwenendo wa timu zao na juhudi wanazozionyesha katika michezo ya VPL, mmojawapo kati ya Tambwe na Msuva anaweza kushinda tuzo hiyo.
Baada ya nyota hao wanne kuna wachezaji watatu ambao kila mmoja amefunga magoli sita, Mzamiru Yassin, Haruna Chanongo na John Bocco.