WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea zaidi ya sh. milioni 760 zikiwa ni misaada kwa wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.
Amepokea misaada hiyo kutoka kwa taasisi na wadau mbalimbali likiwemo kundi la wanawake New Millennium linaloundwa na wake wa viongozi wa Serikali walio madarakani na waliostaafu.
Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika jana jioni (Alhamis, Septemba 29, 2016) kwa nyakati tofauti kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam pamoja na makazi ya Waziri.
Miongoni mwa waliokabidhi misaada hiyo ni pamoja Meya wa jiji la Dar es Salaam Mhe. Isaya Mwita sh. milioni 10, Kampuni ya mabati ya ALFA imekabidhi mabati yenye thamani ya sh. milioni 50 na kampuni ya Bia Tanzania (TBL) sh.milioni 100.
Wengine ni Ofisa Mtendaji Mkuu kampuni ya vinywani baridi ya Pepsi Cola, Bw. Avinash Jha amekabidhi sh.milioni 50, kampuni ya Round Table pamoja na wadau wao sh. milioni 57, kampuni ya Wool Worth sh.milioni 20 na Jumuiya ya Waislam (FIRDAUS) imetoa viti 15 vya walemavu.
Aidha, kampuni ya Trans Ocean Supplies LTD imetoa sh. milioni 20, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza amekabidhi sh. milioni 18.681,Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Shy-Rose Bhanji amekabishi sh. milioni tano.
Pia Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta Tanzania kimekabidhi sh. milioni 415.8, kundi la mtanzao wa kijamii la Whatsapp la Papaso, D’jaro Arungu limekabidhi sh.520,000 na kampuni ya mafuta ya Camel iliyokabidhi mifuko 1,000 ya saruji.
Jumuia ya Wanataaluma ya Vyuo Vikuu vya Umma Tanzania (ASAs) imekabidhi sh. milioni 7.5, Umoja wa Wamiliki wa Maduka ya Dawa Muhimu Tanzania umekabidhi dawa zenye thamani ya sh. milioni tano pamoja na Eric Shigongo wa Global Publisher amekabidhi mabati 500 yenye thamani ya sh. milioni 10.
Waziri Mkuu amewashukuru wadau wote kwa misaada hiyo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.
“Tunashukuru sana kwa michango yote. Michango hii ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo. Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na maafa. Amesema.
Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669(M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616(Tigo Pesa).
Tetemeko hilo lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,