Watumishi watatu wa Serikali akiwamo Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Bukoba, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba wakituhumiwa kutaka kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.
Watumishi hao wanadaiwa kutaka kujipatia fedha hizo baada ya kufungua akaunti feki iitwayo kamati ya maafa Kagera kwa ajili ya kukusanya fedha za kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10 mwaka huu.
Watumishi waliofikishwa mahakamani hapo jana ni aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantus Msole, Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Kelvin Makonda, Mhasibu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai na Meneja wa CRDB tawi la Bukoba, Carlo Sendwa.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Hashimu Ngole, alidai watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa makosa mawili.
Alilitaja shtaka la kwanza kuwa ni kula njama za kutenda kosa la kufungua akaunti feki yenye jina linalofanana na jina la akaunti iliyofunguliwa na Serikali kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi.
Aliitaja akaunti hiyo kuwa ni yenye jina la Kamati Maafa Kagera yenye namba 015225617300.
Kwa mujibu wa wakili huyo, watuhumiwa hao badala ya kutumia akaunti ya Serikali kukusanya fedha za maafa, walifungua akaunti yao waliyoipa jina la Kamati Maafa Kagera yenye namba 0150225617300.
Alilitaja shtaka la pili kuwa ni watuhumiwa kutumia madaraka na vyeo vyao vibaya kinyume cha sheria.
Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao walimwomba hakimu awapatie dhamana wateja wao kwa kuwa bado ni watumishi wa Serikali na wanao uwezo wa kujidhamini wenyewe na hawawezi kutoka nje ya Kagera.
Washtakiwa hao walirejeshwa rumande ambapo kesi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo Septemba 30 na hakimu atatoa maamuzi kuhusu dhamana yao.