SERIKALI imeanza kuchukua hatua za kukabiliana ujenzi holela kwa kutayarisha mipango kabambe ya miji katika miji saba nchini. Miji hiyo ni Mwanza, Musoma (Mara), Singida, Kibaha (Pwani), Tabora, Iringa na Mtwara.
Hayo yalisema bungeni jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alipokuwa anaelezea mikakati ya serikali katika kukabiliana na changamoto ya kupanga miji ili kuondokana na ujenzi holela.
Kauli hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (CCM), aliyetaka kujua ni lini Serikali itatumia wataalamu wake katika kupanga miji na kuondokana na ujenzi holela unaoendelea katika sehemu mbalimbali nchini.
Naibu Waziri alisema mbali ya miji hiyo, mpango kama huo haujatangazwa kwa jiji la Dar es Salaam, huku katika Jiji la Arusha, bado halmashauri mbili za Meru na Arusha, hazijaridhia.
Mbali ya kuandaa mipango kabambe ya miji, alisema wizara inahakikisha kila kipande cha ardhi nchini kinapimwa na kwamba serikali imeshaanza kufanya upimaji katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro na inachukua hatua kuruhusu kampuni binafsi kushiriki katika kutayarisha mipango hiyo.
Alisema wizara pia, ilitoa wataalamu wake katika juhudi za kurasimisha makazi katika Kata za Saranga na Kimara kwenye Manispaa ya Kinondoni na katika Kata ya Tandala, wilayani Makete.
“Katika mwaka huu wa fedha, wizara inatarajia kupeleka wataalamu katika Halmashauri za Manispaa za Sumbawanga, Lindi, Kigoma/Ujiji, Singida, Musoma na Tabora ili kurasimisha pia makazi…” alisema na kuongeza kuwa serikali imeandaa mwongozo wa namna ya kufanya urasimishaji na kwamba utakapokamilika utasambazwa katika halmashauri zote nchini.