SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 26 Septemba 2016

T media news

NMB yaendelea kutoa elimu kupitia mkutano mkuu wa ALAT mjini Musoma

BENKI ya NMB imeendelea kutoa elimu kwa viongozi wa Halmashauri, Manispaa, Majiji na wananchi wa kada mbalimbali juu ya huduma za kibenki ambazo wamekuwa wakizitoa kupitia mkutano mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Tawala na Serikali za Mitaa (ALAT) unaofanyika kitaifa mjini Musoma mkoani Mara ambapo wajumbe zaidi ya 500 wanahudhuria mkutano huo.

Kwenye picha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene akisalimiana na meneja wa NMB tawi la Musoma, Sebastian Kayanga alipokuwa anaingia kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mwembeni Complex kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa mwaka wa ALAT Taifa. NMB imedhamini mkutano wa ALAT Taifa kwa shilingi Milioni 206 ikiwa ni gharama za mkutano na zawadi kwa ajili ya Meya bora wa Mwaka. Pichani kulia ni Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya ziwa, Amos Mubusi.

Kupitia mkutano huo NMB imeelezea jinsi ilivyounganisha mfumo wake wa kibenki na mfumo wa serikali za mitaa (LGRCIS) kufanikisha ukusanyaji mapato ya kwa wakati na bila kupotea na kuandaa vituo vya makusanyo ya fedha kusaidia serikali katika makusano.

Akitoa mada kwenye mkutano huo ulioingia siku ya 2 hii leo,Afisa Mkaguzi Mkuu wa ndani wa (NMB) Augustino Mbogella,amesema licha ya kusaidia serikali katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, benki hiyo pia imesaidia miradi ya maendeleo ya jamii ikilenga zaidi katika utoaji wa misaada katika sekta ya elimu  na afya.

Mbogella amesema mwaka 2015 pekee zaidi ya shule 140 za msingi na sekondari zilipata zaidi ya madawati 7,000 kwa Tanzania nzima katika mpango wa kuendelea kutatua tatizo la madawati mpaka kufikia septemba 2016 tayari wametumia zaidi ya milioni 900. 

“Upande wa afya tumetoa vifaa mbalimbali kwenye hospitali 50 za serikali pamoja na vituo vya afya ambapo kiasi cha fedha takribani shilingi milioni 200 zilitumika” alimalizia Augustino Mbogella.

Wakati huo, viongozi na wananchi wameombwa kutembelea banda la NMB ili kuweza kupata elimu zaidi likiwemo pia suala la ufunguaji wa akaunti mbambali kwenye benki hiyo ambazo zina manufaa makubwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) George Simbachawene,akisaini kitabu cha wageni kwenye banda la NMB kwenye maonyesho ya ALAT.