Beki kisiki wa Yanga na Timu ya Taifa ya Togo, Vincent Bossou akiwa ameanza kwenye kikosi cha kwanza baada ya muda mrefu ameisaidia timu yake ya taifa kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Djibouti katika mchezo wa Kundi A wa kufuzu fainali za Afcon 2017 nchini Gabon.
Bossou ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao kwa Togo baada ya kufunga bao zuri mnamo dakika ya 25, huku Methiu Dossevi akifunga bao la pili.
Mchezaji Kodjo Laba aliifungia Togo bao la tatu mnamo dakika ya 52.
Togo walizidi kushiindilia msumari wa moto kwa Djibouti baada ya kupachika magoli mawili ya haraka-haraka mnamo dakika ya 87 na 90 yaliyofungwa na Komlan Agbegniadan.
Hata hivyo pamoja na ushindi huo mnono, Togo wamemaliza nafasi ya pili kwa kujikusanyia alama 10 nyuma ya vianara Tunisia wenye alama 13.
Kwa upande wao, Tunisia nao pia wameibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Liberia katika mchezo mwingine wa Kundi lao.
Licha ya kipigo hicho Liberia wamesalia na alama zao 10 wakisika nafasi ya tatu, huku wachovu wa Djbouti wakishikilia mkia wakiwa hawana hata alama moja baada ya kupoteza michezo yote.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Togo kupata nafasi ya kushiriki Afcon baada ya mara ya mwisho kufanya hivyo mwaka 2013 wakati walipofika hatua ya robo fainali.