SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 1 Agosti 2016

T media news

Jicho la 3: ‘MSISHANGILIE MABADILIKO YASIYO RASMI HIVI SASA, JIULIZENI PIA NI KWANINI AVEVA AMEKUBALI SIMBA…’

Na Baraka Mbolembole

WAKATI baadhi ya wanachama/mashabiki wa klabu ya Simba SC walipojaribu kutaka kumshambulia mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Poppe mara baada ya timu yao kupoteza 1-0 dhidi ya Toto Africans kisha 1-0 dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa msimu uliopita.

Niliandika makala ya kukosoa mpango huo ‘mbaya’ na badala yake niliwashauri wanachama hao kufanya kila jitihada hata iwe kwa shinikizo kuhakika wanapata mkutano mkuu. Nilisema, Poppe ‘amewekwa’ na rais wa klabu katika timu hiyo, hivyo wanachama walipaswa kuhakikisha Evans Aveva ‘anasarenda,’ na sehemu pekee ya kuonesha nguvu yao ilikuwa ni katika mkutano mkuu wa mwaka wa klabu.

Niliwakumbusha pia kuwa ni wao (wanachama) ndiyo waliompatia nafasi ya urais Aveva kwa maana hiyo ni wao pia walikuwa na mamlaka ya kumuwajibisha na bila shaka nasema kati ya ‘malipo mengine makubwa kuyapata’ basi haya yaliyofanywa na wanachama wa klabu hiyo katika siku ya mwisho kabisa ya mwezi Julai, jana Jumapili.

Wanachama wengi walipaza sauti huku wakitaja jina la Mohamed Dewji ‘MO’ kwa maana hiyo hawakuwa na mtazamo mwingine wowote ule wala kutafakari ni kwanini wamekwama hapo walipo kwa miaka 80.

Kiukweli umefika wakati wa Simba kuondoka katika mfumo wa sasa wa uanachama na kuwa kampuni kwa maana nimejifunza zaidi katika mkutano wao wa jana ni jinsi gani timu hiyo itakavyoendelea kuwa. Huwezi kubadilisha mfumo ulioutumia kwa miaka 80 ndani ya mwaka mmoja au miwili baada ya kuibuka kwa mpango wa mabadiliko.

Bahati mbaya wanachama wenyewe wengi wao si wapembuzi. Wanasoka wengi wanahitaji mpango huo lakini ni kwanini MO ametumia nguvu kubwa kushinikiza kuhusu mabadiliko-kutoka utaratibu wa kadi hadi soko la hisa?

Timu itakuwa ni ya wafanya biashara wachache wenye mtazamo mkubwa, na si hivyo itakuwa chini ya ‘wafanyabiashara wa kimataifa’ na kuondoka katika utegemezi wa ‘wafanyabiasha wa kitaifa’ ambao kwa miaka 80 ‘labda’ wameitumia kujinufaisha wao binafsi na kuicha klabu hiyo vilevile kwa tangu ilipoanzishwa mwaka 1936.

Tangu mwaka 2012 nimefuatilia kwa ukaribu kabla na baada ya mikutano ya klabu hiyo (ukiwemo ule wa uchaguzi uliowaingiza madarakani rais Aveva, Makamu wake Geofrey Nyange Kaburu na timu yao ya uongozi mwaka 2014).

Na baada ya uamuzi wa jana ni wazi kundi kubwa la wanachama wa klabu hiyo hawawezi hata kuwa na msaada wa kimawazo ni namna gani timu yao inaweza kupata mafanikio katika mfumo wa sasa. Ni makosa.

Yaani, mfano katika wanachama 1000, wanachama kumi tu ndiyo wawe na upeo mkubwa, kipi unategemea? Ni kupata viongozi ‘bomu’ kutoka katika wanachama wasio na mawazo bora ya kimaendeleo.

Hapo hamuwezi kuendelea. Na ndipo unapoona matajiri wakijitokeza wakiitamani klabu hiyo kwa maana ni taasisi kubwa iliyoanzishwa hata kabla ya uhuru na watu wamekuwa wakiipenda kizazi hadi kizazi.

Aveva amefeli, na hata katika shabaha yake kuu ya kuombea kura katika uchaguzi wa mwaka 2014 imeshindwa vibaya mno.

Sera ya pointi ingemsaidia pia kiuchumi kama angefanikiwa kwa maana watu wangeenda uwanja lakini mpango wake wa kutumia nembo ya klabu hiyo na kupeleka bidhaa sokoni umekuwa na faida ndogo kwa watu wachache huku klabu ikishindwa kunufaika na chochote kiuchumi.

Kama ndoto ya MO itatimia, hata mimi nitakuwa nanunua kibiriti chenye nembo ya Simba SC kwa maana nitakuwa naingiza ka-faida kidogo katika akaunti ya mwanahisa mkuu wa klabu ninayoishabikia. Namaanisha hakutakuwa na biashara za ujanjaujanja. Sijawahi kununua jezi ya klabu yoyote ile ya Tanzania lakini kwa miaka 16 sasa jezi ndiyo nguo isiyobanduka mwilini mwangu.

NI KWELI AU AVEVA ALITUMIA SIASA ILI KUONDOKA SALAMA

Kwa hali jinsi ilivyokuwa endapo Aveva angekataa mpango wa kundi kubwa la wanachama lililohitaji mabadiliko mambo yangekuwa si mambo kwa maana mkutano aliousifia mwishoni ungekuwa uwanja wa vita.

Lugha yake ya mwili ilionekana ameliingia na mpango wa kuyakataa mabadiliko na ndiyo maana unaona kule Bunju kulikuwa na makatapila yakifanya kazi ya kuondoa visiki na kusawazisha vifusi katika uwanja wao.

Kwanini wamelenga kazi hiyo kuanza wikendi ya mkutano mkuu? Wamefeli kwa mara nyingine katika ‘ahadi’ waliyokuwa wameiandaa. ‘Uungwana ni vitendo’ na sidhani kama Aveva alikubaliana na mpango wa mabadiliko ili apate nafasi ya kuondoka salama katika mkutano huo.

Pia siamini kuwa utawala wake utashindwa kukubaliana kwa vitendo na mabadiliko hayo ya kutoka klabu ya wanachama hadi kampuni. Simba wako katika hatua nzuri sasa lakini bado siamini katika uharaka na shinikizo lililotumika ili pande mbili kuungana kimtazamo.

Jicho langu la Tatu linaona bado Simba haijafikia malengo ya kuwa kampuni hadi pale nyaraka muhimu zitakaposainiwa na mabadiliko hayo kuwa rasmi.

Msishangilie mabadiliko yasiyo rasmi hivi sasa, jiulizeni pia ni kwanini Aveva amekubali Simba SC kutoka katika mfumo wao wa miaka 80 na kuwa kampuni. Kwanini Aveva ameshindwa? Kwanini MO ameshinikiza kuhusu mabadiliko?

Baada ya Simba SC Day ntamalizia ‘jicho langu la tatu’ ambalo linaona siasa kuliko uhalisia katika mabadiliko yanayotegemewa. Usiwaamini sana ‘Mafionso-Genge la wahuni.’

Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu #BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.