SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 28 Julai 2016

T media news

Mwigulu Awatia Mbaroni Mchina, Watanzania Waliomtesa Kijana Mgodini


Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (wa pili kushoto) akiwa katika Gereza la Wilaya ya Geita.

Mhe. Mwigulu akimkagua majeraha kijana aliyeteswa mgodini.

Mhe. Mwigulu akiwa eneo la mgodi pamoja na kijana aliyeteswa ili awatambue watuhumiwa.

  

Zoezi la kuwatambua watuhumiwa likiendelea.

Waziri Mwigulu akiwa na mmoja wa watuhumiwa.

Watuhumiwa wakiwa chini ya ulinzi.

…Wakishuka kutoka kwenye difenda.

Picha iliyoenea mitandaoni ikimuonesha kijana huyo akipigwa na Mchina mgodini.

Na Johnson James / GPL

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba jana amewasili mkoani Geita kwa ziara ya kikazi kubwa ikiwa ni kufuatilia taarifa za mateso na mauaji yaliyofanywa na raia wa China wanaomiliki sehemu ya mgodi wa Nyamhuna uliopo Katoro-Geita dhidi ya wafanyakazi/vibarua ambao ni Watanzania.

Takribani wiki moja sasa kumekuwa na hali ya sintofahamu dhidi ya picha zinazoenea mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zikionesha raia wa Tanzania anayefanya kazi kwenye mgodi tajwa akiteswa na kufanyiwa vitendo vya kinyama na mwajiri wake ambaye ni raia wa China.

Ilimlazimu waziri mwenye mwenye dhamana na usalama wa raia na mali zao kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kufika eneo la mgodi kujiridhisha kwa taarifa zilizotapakaa na kubeba simanzi kwa Watanzania.

Mwigulu Nchemba amejiridhisha kuwa kulikuwepo na tukio hilo la Mtanzania kuteswa na huyo mwajiri wake kipigo kilichopelekea kupoteza fahamu na siyo kifo.

Hatua za awali, alizozifanya Mhe. Mwigulu  ni kwenda Gereza la Wilaya ya Geita alikohifadhiwa kijana huyo kwa madai ya kushitakiwa na mwajiri wake kwa kosa la wizi lililopelekea yeye kupigwa.

Katika mahojiano ya Waziri Mwigulu Nchemba na kijana huyo, Mwigulu alibaini kuwa kijana huyo aliyepo gerezani ndiye mhanga wa tukio lile kwa uthibitisho wa makovu yaliyopo mwilini mwake na mavazi aliyovalia wakati anateswa na wakati yupo hapo gerezani.

Kutokana na hali hiyo,  ilimlazimu Mh. Mwigulu kwenda mgodini akiwa ameambatana na kijana huyo kwa ajili ya kutambua waliofanya vitendo hivyo vya kinyama. Katika oparesheni hiyo, kijana  aliyeteswa na kujeruhiwa aliwabaini Watanzania watano ambao ni walinzi wa eneo hilo na Mchina mmoja walioshirikiana kumpiga, kumtesa na kumjeruhi.

Kufuatia utambuzi huo na maelezo ya wahusika, Nchemba akaagiza wahusika wakamatwe mara moja na aliondoka nao kwa hatua zaidi za kisheria.

Katika hali nyingine ya kusikitisha, Mwigulu amebaini uwepo wa wahamiaji haramu raia wa China katika mgodi huo ambapo nyaraka za uhamiaji Mkoa wa Geita zinaonesha raia 28 wenye vibali ndiyo walioruhusiwa kukaa kwenye mgodi huo, lakini katika operesheni hiyo ya kushitukiza aliyoifanya Mh. Mwigulu  alibaini uwepo wa raia wa China zaidi ya 50 wanaoishi katika mgodi huo kinyume na sheria. Hivyo amemuagiza mkuu wa mkoa na timu yake ya uhamiaji kuhakikisha wote wasio na vibali wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria