Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp, ametanabaisha sababu za kumrudisha nyumbani beki wake Mamadou Sakho badala ya kubaki naye katika kambi waliyoweka nchini Marekani.
Klopp amesema kwamba Sakho, ambaye hivi karibuni aliondolewa adhabu yake ya kufungiwa kutokana na tuhuma za matumizi ya madawa ya kusisimua misuli, alivunja sheria za klabu hiyo mara tatu na sasa ana hatihati ya kutemwa ikiwa kocha huyo atachukua maamuzi mazito zaidi.
“Ilikuwa ni almanusura achelewe ndege ambayo ilikuwa ikibeba timu kutoka Liverpool kwenda San Francisco, alikosa kufanya mazoezi na timu na pia alichelewa kujumuika na wenzake kupata chakula,”alisema Klopp
Natakiwa kutengeneza kikosi hapa na tunapaswa kuanzia hapa. Nilidhani pengine kulikuwa na ulazima wa yeye kurudi Liverpool sasa.
“Tuna sheria zetu hapa ambazo tunapaswa kuziheshimu, kama kuna mtu naona hafanyi hivyo, lazima nichukue hatua.
Baada ya siku nane au kumi tunaweza kuzungumza juu ya hilo. Hatukuwa na mazungumzo yoyote lakini nilimweleza, huwezi kujibana wakati anayeongea ni mtu mmoja.”
Alipoulizwa kama Sakho atapigwa faini, Klopp alisema angependa kuona adhabu mbadala ikichukuliwa kwasababu asingependa kukurupuka kutoa maamuzi.
“Kumpiga faini? Unaweza kuuliza, na naweza kulielezea hilo kwa undani zaidi,” alisema Mjerumani huyo.
“Sipendezewi na adhabu za kutoza wachezaji fedha, kiukweli hii haitokei mara kwa mara kwenye maisha yangu, naweza kumpiga faini mtu yoyote lakini sipendi kwasababu nataka tuwe na nidhamu, tujifunze pamoja na kufanya yaliyo sahihi.
“Sehemu zote ambazo nimepita, huwa sipendi utaratibu huo, ni jambo la kufurahisha, lakini unapompiga mtu faini halafu akarudia kosa utakuwa umemsiadia nini, mara nyingi faini huwa haisaidii.
“Si kana kwamba wanajali sana pesa, ila unakuta wakati anatoa pesa anakuwa anaumia lakini baada ya muda anasahau. Hivyo, nataka wachezaji wote wafuate yale yote ambayo yapo kwenye utaratibu wetu.”