RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amesema kuwa mara baada ya kustaafu Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anapumzika na hayuko tayari kufanya shughuli za kichama na kiserikali.Aidha amesema kuwa yuko tayari kutoa ushauri kwenye shughuli za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kilimo na mifugo.
Aliyasema hayo mjini Bagamoyo kwenye ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo wakati wa sherehe za kumkaribisha baada ya kustaafu na kumkabidhi nafasi ya uenyekiti Rais John Magufuli.
Kikwete alisema anamshukuru Mungu kwa kuwa katika kipindi chake, ameongoza na kuiacha nchi ikiwa na utulivu mkubwa licha nchi kupitia kwenye kipindi kigumu.
“Namshukuru Mungu kwani nchi iko salama na chama kiko imara nami kwa sasa nataka nipumzike sitajihusisha tena na masuala ya kisiasa au kiserikali nataka nipumzike,” alisisitiza Kikwete.
Aliendelea kusema, “mkija kwa ajili ya suala la maendeleo niko tayari lakini kwa suala la kutoa ushauri kuhusu serikali hapana... kwani kwa sasa kuna viongozi ambao wana uwezo...mimi nataka nipumzike.”
Awali wabunge wa mkoa huo wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa watamuenzi Kikwete kwa kujenga mnara wa kumbukumbu kwenye Ofisi ya CCM mkoa wa Pwani kwenye mti wa Mkungu Maarifa ambapo ndipo alipotangaza kuwania urais kupitia chama hicho.
Kawambwa alisema kuwa ujenzi huo utaanza mara moja na watamwalika kuuzindua mara utakapokamilika. Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani, Joyce Masunga alisema kuwa viongozi wa mkoa huo unampongeza kwa kuiongoza nchi na kuiletea mafanikio makubwa