SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 29 Julai 2016

T media news

JAVIER MASCHERANO – NAHODHA ASIYEVAA KITAMBAA UWANJANI

Katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi, Barcelona wamepoteza mchezaji mmoja ambaye amekwenda Juventus. Si mwingine bali ni Dani Alves, huyu aliitummikia Barcelona kwa uaminifu mkubwa kwa kipindi cha miaka nane. Baada ya Alves ilionekana kama vile Javier Mascherano naye angeunga tela, lakini sio kama wengi walivyotaraji. Barcelona wameamua kumbakisha kitasa huyo raia wa Argentina. Na hii naweza kusema kwamba ni habari njema sana kwa mashabiki wa Barcelona na bosi wao Luis Enrique.

Wiki iliyopita Enrique alikiri kwamba ameshangazwa sana na kitendo cha Alves kuondoka klabuni hapo. “Nachoweza kufanya mimi ni kumpongeza tu,” alisema. “Namtakia kila la heri, ni moja ya wachezaji bora sana amba nimewahi kuwashuhudia katika maisha yangu ya soka. Juventus wamelamba dume kwelikweli kwa kumpata Alves.”

Ikumbukwe tu kwamba baada ya kumsajili Alves, Juventus pia walikuwa wanaimendea saini ya Mascherano, lakini Barca wakaona hapana isifikie hatua hii. Alves alinukuliwa akisema angependa sana kucheza tena na Mascherano. Hiyo kauli ya Alves iliwashtua sana Barca na mara moja wakaamua kumvika kitanzi Mascherano ili aendelee kuitumikia klabu hiyo kwa kipindi kingine tena.

“Klabu imenipa taarifa kwamba isingependa kuona naondoka, wanafuraha sana na uwepo wangu hapa,” Mascherano alisema mwezi uliopita. Na baada ya kidogo tu Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona Robert Fernandez akaahidi kwa kusema: “Mascherano ataendelea kuwa mchezaji wa Barcelona. Nina uhakika na hilo na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha suala hili linatimia.”

Sasa suluhisho lenyewe limefikia tamati Jumatano wiki hii ambapo Barca walitangaza kwamba kiungo huyo wa zamani wa Lverpool amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu. “Javier Mascherano ataendelea kutoa huduma yake hapa Barcelona kwa miaka mitatu zaidi,”ilisomeka taarifa kutoka kwenye Twitter ya klabu ya Barcelona.

Unajua nini hasa kimefanya Mascherano aongezewe mkataba? Kumbuka kiungo huyu aliletwa na Pep Guardiola mwaka 2010 baada ya kupendekezwa na Messi. Mascherano kwa mara ya kwanza kabisa alicheza kwenye mchezo dhidi ya Hercules ambapo Barca walikufa 2-0 nyumbani. Baada ya mchezo huo alikosolewa vikali na mashabiki kwa kiwango alichoonesha, lakini sababu kubwa ilikuwa ni kwamba hakuwa bado ameweza kuendana na mfumo wa klabu yake hiyo mpya. Hata hivyo pia alibadilishwa kutoka kucheza kiungo mpaka beki wa kati.

Guardiola aliona faida ya Mascherano kucheza kama beki wa kati na kuamini kwamba angeweza kufanya hivyo baada ya muda. Alimwamini sana kwa kuwa aliiona ari ya uongozi aliyonayo mchezaji huyo pindi awapo uwanjani akishirikiana kwa uzuri na beki kisiki wakati huo Carles Puyol na baadaye kutengeneza safu imara na Gerard Pique. Mascherano amekuwa moja ya mabeki bora sana katika ligi za Ulaya ukilinganisha na asili ya nafasi yake na umbo lake pia. Amekuwa ni mfano wa kuigwa. Kwa namna anavyocheza uwanjani amekuwa ni kama nahodha asiye na kitambaa.

“Klabu imesajili mchezaji ambaye, mimi kama kocha nisingeweza kubadilishana na mchezaji mwingine yeyote yule,” alisema Guardiola mwaka 2012. “Kamwe siwezi kumuuza. Ni usajili wa kipekee huu na tuna furaha kubwa sana kujumuika naye pamoja.”

Kama unavyoona bado yupo. Na wakati Luis Enrique alipokuwa akitambulishwa mwaka 2014 alisema jambo hilo hilo kama alilosema Guardiola. Alipoulizwa juu ya Muargentina huyo, aliwaambia waandishi: “Masherano ni kama Xavi. Ni mchezaji muhimu sana, pia kwa sababu ya busara zake akiwa ndani ya nje ya uwanja. Ni mfano mzuri wa namna jinsi nahodha anavyopaswa kuwa.”

Ni kweli, si kwenye timu yake ya taifa wala klabu yake ya Barcelona, Mascherano sio nahodha. Lakini shughuli yake uwanjani kila kocha angependa kuwa na mtu kama huyu. Ni mchezaji ambaye anawaweka mabegani wachezaji wenzake wote. Ni mfano wa kocha mchezaji, kocha anayefunisha huku akicheza. Mtu ambaye wachezaji wenzake wanamuangalia wakati timu ikiwa na shida. Si mtu ambaye anahitaji kuwa na kitambaa begani ili kuwa nahidha, yeye ni nahodha tosha bila hata ya kuvaa kitambaa begani. Barcelona hawajafanya kosa na wala hawatajutia kumwongezea mkataba mwingine wa kuitumikia klabu hiyo.

Unaikumbuka ile fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ujerumani mwaka 2014? Licha kwamba Messi ndiye alikuwa nahodha uwanjani lakini kazi aliyoifanya Mascherano ilitosha kuthitibisha uongozi wake uwanjani.

Alifanya kazi kubwa sana ya kuwapa morali wachezaji wenzake pamoja, na kufanya kazi kubwa ya kupunguza kasi ya mashambulizi langoni mwao kutokana na kukaba kwa umakini wa hali ya juu, hasa kulingana na nafasi yake ya kiungo mkabaji aliyokuwa akicheza. Huyu ndiyo Javier Mascherano, kiungo aliyebadilishwa mpaka kuwa beki kitasa Barcelona.