Bara la Afrika litatunukiwa nafasi nyengine mbili zaidi iwapo dimba la dunia litaongeza idadi ya mataifa yanayoshiriki hadi 40 kuanzia mwaka 2026 kulingana na rais wa FIFA, Gianni Infantino.
Infantino alipendekeza kuongezwa kwa timu hizo kabla ya kuchaguliwa kwake na shirikisho hilo la soka duniani. Kwa sasa Afrika ina nafasi tano pekee katika michuano hiyo .
“Pendekezo langu limekuwa timu 40 na iwapo hilo litadhinishwa pendekezo langu ni kulipatia bara la Afrika nafasi mbili zaidi,” alisema Infantino.
Hata hivyo hatua hiyo itaidhinishwa hadi mwaka 2026 huku timu 32 zikiwa tayari zimethibitishwa kushiriki katika kombe la dunia la 2018 nchini Urusi na 2022 nchini Qatar.
Source: BBC