SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 2 Mei 2016

T media news

Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein Aapishwa Rasmi Kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein leo asubuhi tarehe 02 Mei, 2016 ameapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri ili aweze kushiriki na kutekeleza majukumu yake ndani ya Baraza hilo.

Rais Shein ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma, tukio ambalo limeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Viongozi wengine walioshuhudia tukio hilo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo mchana ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Mawaziri, uliopo Ofisi ya Rais TAMISEMI Mjini Dodoma.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
02 Mei, 2016