Masoud Kipanya amerejea tena Clouds FM baada ya miaka minane kuondoka. Mchoraji huyo maarufu wa katuni ya Kipanya, anasikika kwenye kipindi cha Power Breakfast.
“Sijui kama unajua kuwa mimi Clouds nilifukuzagwa kazi! Msingi wa kutoka Clouds ni kwamba sikutoka kwasababu nilikuwa labda niko hivi hapana, tulikuwa tunafanya kazi zetu kama kawaida baadaye kuna mambo yaliyotokea tukaonekana [Yeye na Fina Mango] ni watovu wa nidhamu tukafukuzwa,” alisema Masoud kwenye kipindi cha Danga Chee cha Channel Ten.
“Kwahiyo I was fired, nilifukuzwa kazi. Sasa miaka minane baadaye watu hao hao wakikuapproach kufanya nao kazi kwa terms ambazo mnakaa chini sasa kama watu wazima, watu ambao wanaona kabisa kwamba miaka minane umekaa bila wao na ya kwako yanakuendea. Kwanza hapo kuna heshima kubwa sana, katika hali ya kawaida nilitakiwa niwe nimeshadondoka, sipo, sifai, siwezekani tena. Lakini kama watu wamekuona kwamba unahitajika kwenye ile sehemu ni kipimo kingine cha kuonesha kwamba ‘okay kumbe kitendo cha kubaki kwenye media kama mchoraji katuni thamani iko pale,” aliongeza.
“Lakini namba mbili ni kwamba ninapofuatwa nirudi Clouds, tumekaa mezani tumezungumzia masuala ya mkwanja wa kutosha, wakati huo huo project zangu zote hakuna hata moja inayovunjika, kuna tatizo gani mimi kutengeneza extra money katika masaa matatu au masaa manne?”