MKUU wa Mkoa wa Dares Salaam, Paul Makonda amewasainisha mkataba wakuu wote wa idara kusimamia na kuhakikisha hakuna mtumishi hewa atakayebainika kwenye idara zao.
Katika utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilotoa Machi 15 mwaka huu kwa wakuu wa mikoa kufuatilia na kubaini watumishi hewa, Mkoa wa Dar es Salaam umebainika kuwa na watumishi hewa 209 walioisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni mbili.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, Makonda alisema hayupo tayari kuendelea kuona watumishi hewa wanaendelea kuwapo.
Alisema ni jukumu la kila mkuu wa idara kuhakikisha anasimamia eneo lake. Makonda alisema mkataba utaanza kazi rasmi baada ya siku saba.
Alisema baada ya hapo, atakayebainika kuwa na mtumishi hewa, atawajibika katika kulipa gharama zote za hasara alizoingiza kwa malipo yatakayofanyika.
“Nataka ndani ya siku saba hizi mpitie upya, mhakiki watumishi wenu baada ya hapo sitataka kusikia sababu yoyote lazima tufanye kazi kila mmoja kwa nafasi yake na msisubiri kila kitu msimamiwe,” alisema Makonda.
Pia aliwataka wakuu hao kuhakikisha kila mwisho wa wiki wanampelekea taarifa ya kila idara jinsi watakavyofanya kazi.
Wakuu wa Idara mbalimbali wa Manispaa za jiji la Dar es Salaam wakisaini mkataba wa kutafuta watumishi hewa katika manispaa zao jijini Dar es Salaam, na atakaye shindwa kuwafichua baadae wakija kujulikana atawajibishwa yeye.
Wakuu wa Idara mbalimbali wa Manispaa za jiji la Dar es Salaam wakiapa kiapo cha mkataba wa kutafuta watumishi hewa katika manispaa za jijini la Dar es Salaam jana walipo apishwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.