Mtumishi wa Wizara ya Fedha, Aneth Msuya (30) ambaye ni mdogo wa Bilionea Erasto Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi 22 KIA, ameuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake eneo la Kigamboni jijini Dar Es Salaam.
Mmoja wa ndugu wa familia hiyo, Shujaa Khamis, jana alithibitisha kuuawa kwa Aneth, lakini alikataa kuingia kwa undani.
“Ni kweli wamemchinja usiku wa kuamkia leo (jana) na hapa nipo kwenye msiba hapa nyumbani (Mererani) kwa baba. Tumeambiwa wamechukua Tv tu,”alisema.
Hata hivyo, Khamis alikataa kueleza lolote kama wana mashaka na mauaji hayo zaidi ya kuliomba Jeshi la Polisi nchini, kuchunguza kiini cha mauaji hayo na kuwasaka waliohusika.
Habari nyingine kutoka Wizara ya Fedha, ziliwakariri baadhi ya watumishi wakisema wamepata taarifa za msiba huo, lakini hawajapewa taarifa rasmi.
“Tuna taarifa tunazisikia sikia kuwa ameauawa, lakini jana (juzi) tulikuwa naye kazini ila leo (jana) ndiyo tunasikia amechinjwa na watu wasiojulikana. Imetusikitisha sana,” alisema mmoja wa watumishi hao ambaye hakutaja jina kwa kuwa si msemaji.
Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Andrew Satta alipofutwa jana kuthibitisha taarifa za mauaji hayo alisema yuko kwenye kikao.